Mwanamke mmoja anayefahamika kwa jina la Enea Mkimbo (55) Mkazi wa Kihesa Kilolo Manispaa ya Iringa, amejinyonga leo September 14,2022 chanzo kikidaiwa kuwa ni kuzidiwa na madeni ya VICOBA na usumbufu kutoka kwa Wanakikundi wenzie.
Mwenyekiti wa Mtaa huo Michael Mlalwe amesema Marehemu Enea ambaye ameacha Mume na Watoto watano, jana September 13,2022 alifuatwa na Wanakikundi wakimshinikiza kutoa pesa ambapo baada ya tukio hilo Enea alimuaga Mumewe kuwa anaenda kulala kwa Mama yake mzazi eneo la Ilembila na badala yake aliingia jikoni na kujinyonga kwa kutumia kitenge.
Mwenyekiti huyo amesema Serikali ya Mtaa inapanga kuwaita Wanakikundi ili kujua walizungumza nini na Enea mpaka kufikia hatua ya kujitoa uhai wake.
Kufuatia tukio hilo Wananchi wa Mtaa huo wameiomba Serikali kuangalia upya uwepo wa Taasisi zinazotoa mikopo kwa riba kubwa inayoumiza Wananchi maarufu kama mikopo ya moto ambayo imekua ikichangia Watu kujitoa uhai.
Source: Millard Ayo