Mwalimu wa shule ya msingi Kyawazaru, iliyopo wilayani Butiama mkoani Mara, Idrisa Athuman Najela, amehukumiwa kifungo cha maisha jela na Mahakama ya wilaya ya Musoma, baada ya kupatikana na hatia ya kumlawiti mwanafunzi.
Akisoma hati ya mashtaka Mwendesha Mashtaka wa Serikali Gaston Kayombo, mbele ya Hakimu Mkazi Mwandamizi Khadija Masala, amesema Idrisa Naleja alitenda kosa hilo kwa mwanafunzi huyo mwezi Aprili mwaka 2022 kwa nyakati tofauti ambapo mara ya kwanza alimlawiti ilikuwa katika shamba lililopo karibu na shule ya Kywazaru na mara ya pili ni ofisini kwake baada kuondoka kwa walimu na wanafunzi.
Katika kesi hiyo ya jinai namba 54 ya mwaka 2022 Jamhuri ilikuwa na mashahidi sita akiwemo mhanga wa tukio hilo na Daktari aliyethibitisha kufanywa kwa tukio hilo baada ya vipimo mbalimbali vya kitabibu.
Mwalimu huyo amehukumiwa hukumu ya kesi moja kati ya kesi nane zilizokuwa zikimkabili, ambapo kesi saba bado hazijatolewa uamuzi na hii baada ya kufanya vitendo vya ulawiti kwa wanafunzi nane wa shule hiyo.