Na Said Muhibu, Lango La Habari
Sekretarieti ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) imewafungulia mashtaka ya kimaadili Rais wa klabu ya Young Africans Sports Club Mhandisi Hersi Said na aliyekuwa Ofisa wa habari na Msemaji wa klabu hiyo Haji Sunday Manara kwa makossa ya kutoheshimu maagizo ya TFF juu ya adhabu aliyopewa Manara ya kutojihusisha na shughuli yoyote ya mpira wa miguu ndani na nje ya nchi.
Taarifa iliyotolewa na TFF leo Jumapili August 07, 2022 imesema Manara ameshindwa kutekeleza adhabu aliyopewa na Kamati ya Maadili ya TFF kutokana na kujihusisha kwenye Sherehe za Tamasha la Siku ya Wananchi hapo jana akiwa kama MC aliyewatambulisha wachezaji wapya na wenyeji kwenye sherehe hiyo.
Hata hivyo Manara alijitetea hapo jana ya kwamba uwepo wake kwenye sherehe hiyo hauhusiani na masuala ya Mpira wa Mguu na kusema yeye ni kama MC wa mtaani tu.
“Mimi sijihusishi na masuala ya michezo hapa, nimelipwa tu kama MC wa kujitegemea. Yaani mimi ni MC wa mtaani tu tena nikimaliza hapa naenda kuwa MC kwenye harusi hapo kigogo,” alisema Manara wakati akiwatambulisha wachezaji wa Yanga.
Aidha, kwa upande wa Mhandisi Hersi Said amefunguliwa mashtaka ya kimaadili kwa kwenda kinyume na kutoheshimu uamuzi uliofanywa na TFF kwa kuruhusu kutokea kwa jambo hilo huku akienda kinyume na Katiba ya TFF ibara ya 16 (1) (a) na Katiba ya Yanga.
Mwenyekiti wa Kamati ya Maadili ya TFF tayari amepelekewa mashtaka hayo, walalamikiwa watapewa mashtaka hayo na mwito mara baada ya Kamati hiyo kupanga tarehe ya kusikilizwa mashtaka hayo.
TFF ilimpa adhabu Manara ya kutojihusisha na shughuli yoyote ya mpira wa miguu mnamo Julai 21, 2022 kutokana na kumdhalilisha Rais wa TFF Wallace Karia siku ya Jumamosi Julai 2, 2022 kwenye uwanja wa Sheikh Amri Abeid, Arusha wakati mechi ya Fainali ya Kombe la Shirikisho la Azam (ASFC) kati ya Yanga dhidi ya Coastal Union ikiendelea.