Wizara ya Maendeleo ya Jamii,Jinsia, Wanawake na Makundi Maalumu imejipanga kuweka mkakati kwa wale wote wanaofanya ukatili wa watoto na wanawake wasipate dhamana ili kuzuia kufanya matukio mengine wakiwa uraiani.
Hayo yamesemwa na Naibu Waziri wa Wizara hiyo Mhe. Mwanaid Khamis kwenye ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Ikungi wakati akipokea taarifa ya Wilaya hiyo iliyotolewa na Mkuu wa Wilaya Mhe. Jerry Muro.
Mhe. Mwanaid amesema kuwa mkakati huo utajikita na kuweka sheria ya kutokuwapatia dhamana kwa mtu yeyote atakayefanya ukatili wowote kwa wanawake na watoto nchini ili wale wanaofanya matukio hayo wasipate dhamana ili kuepusha matukio mengine pale watakapokua uraiana.
"Inasikitisha sana na ukatili unaoendelea hivi sasa nchini, nina imani hatua kali za kisheria zitachukuliwa kwa wale wote wanaofanya matukio ya kikatili ikiwemo ya kutoa uhai ".
Awali akitoa taarifa kwa Naibu Waziri huyo Mhe. Jerry Muro alisema Wilaya yake imejikita kutoa elimu ya kupinga ukatili wa kijinsia kwa kushirkiana na Mabalozi wa SMAUJATA hususan kipindi hiki cha mavuno ambapo kumekuwepo na matukio ya mauaji ya wanawake katika maeneo ya vijijini.
"Tunapambana nao wale wote wanaofanya ukatili kwa watoto na wanawake tunahakikisha tunawakamata,tangu matukio haya yanayotokea kwenye Wilaya yetu tumewakamata wale wote wanaofanya ukatili huu na tunazidi kutoa elimu na Shujaa wa Maendeleo na Ustawi wa Jamii".
Hivi karibuni wanawake wawili kutoka vijiji tofauti katika Wilaya ya Ikungi wameuliwa kikatili na wanaume zao.