Katika kuelekea Kilele cha Maadhimisho ya Miaka 50 tangu kuanzishwa kwa Shirika la Madini la Taifa (STAMICO), Waziri wa Madini Dkt. Doto Biteko amepongeza jitihada na ubunifu unaofanywa na shirika hilo.
Dkt. Biteko ametoa pongezi hizo baada ya kutembelea kiwanda cha kuzalisha mkaa mbadala wa kupikia unaojulikana kama Rafiki Coal Briquettes unaotokana na makaa ya mawe kilichopo jijini Dar es Salaam.
Dkt. Biteko amesema, pamoja na Serikali kuendeleza juhudi za kupambana na matumizi ya mkaa utokanao na misitu na badala yake kutumia nishati mbadala, STAMICO imeunga mkono jitihada hizo kwa kuanzisha kiwanda cha kuzalisha mkaa wa mawe kwa ajili ya matumizi ya kupikia majumbani.
Aidha, Dkt. Biteko amesema kwa sasa STAMICO ina jumla ya uwekezaji wa zaidi ya kiasi cha shilingi bilioni 63.1 ukilinganisha na miaka michache iliyopita ambapo Shirika lilifisika na kutaka kufungwa.
Pia, Dkt. Biteko amesema STAMICO imeagiza mitambo mipya 11 kwa ajili ya uchorongaji na mitambo 4 kwa ajili ya kuzalisha makaa ya mawe ili kuongeza uzalishaji wa makaa hayo na kukidhi mahitaji ya watanzania ambapo mitambo hiyo itasimikwa jijini Dodoma, Songwe, Pwani na Kanda ya Ziwa.
Naye, Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa STAMICO Dkt. Venance Mwasse amesema, Shirika hilo lina mkakati wa kuhakikisha kunakuwa na uzalishaji wa kutosha ili kukidhi mahitaji ya watanzania ambapo limeagiza mitambo miwili yenye uwezo wa kuzalisha tani 20 za makaa hayo kwa saa.
Dkt. Mwasse amesema, mradi huo unatarajia kuwanufaisha watanzania kwa kutoa ajira na utapunguza janga la ukataji miti kwa ajili ya mkaa hivyo kuchangia kutunza mazingira.
Dkt. Mwasse amesema STAMICO imeanza kusambaza nishati hiyo ambayo ni nafuu zaidi na rafiki kwa mazingira baada ya kuidhinishwa na Shirika la Viwango la Taifa (TBS) tayari kwa matumizi baada ya uzalishaji wa majaribio kufanyika kwa ufanisi.
Aidha, Dkt. Mwasse amesema mkaa huo una faida lukuki na baadhi amezitaja kuwa ni pamoja na rafiki wa mazingira, kuokoa pesa nyingi zinazotumika kwenye nishati nyingine, mkaa wa mawe wakupikia unadumu jikoni kwa muda mrefu kuliko mkaa wa miti hivyo kuzidi kupunguza gharama za matumizi ya nishati hiyo, huboresha usafi wa jikoni na maeneo ya nyumbani yanayochafuliwa na mkaa wa miti.
Pamoja na mambo mengine, Dkt. Mwasse amesema, misitu ni muhimu kwa maisha ya binadamu na viumbe hai kwa kuwa huifadhi vyanzo vya maji, kuboresha hali ya hewa, kuzuia mmomonyoko wa ardhi, malisho ya mifugo, kuboresha shughuli za kilimo na kuboresha mandhari ya nchi mijini na vijijini ambapo amewataka watanzania kuunga mkono matumizi ya makaa hayo ambayo matumizi yake ni rahisi na hupika kwa haraka zaidi na yana faida nyingi kuliko mkaa wa miti ambao athari zake kimazingira ni kubwa.
Dkt. ameongeza kuwa, kutokana na manufaa ya mkaa huo, tayari STAMICO inaendelea kuweka mikakati ya kuhakikisha kuwa jamii kubwa inanufaika na inatumia mkaa huo ambao ni wazi utasaidia kufanikisha kampeni ya utunzaji wa misitu ambapo kwa kuzingatia umuhimu wake, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Philip Isidor Mpango anatarajiwa kuuzindua rasmi mkaa huo Agost 12, 2022 ili uanze kutumika rasmi na watanzania wote.