Na Lucas Raphael,Tabora
WAKALA wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) wamepongezwa kwa kutekeleza miradi ya maji vijijini kwa weledi mkubwa na kutatua kero ya upatikanaji huduma ya maji safi na salama katika maeneo mengi.
Pongezi hizo zimetolewa juzi na Mkuu wa Mkoa wa Tabora Balozi Dkt Batilda Burian katika kikao kazi cha kuwajengea uelewa wa pamoja Watendaji wa RUWASA na Sekretarieti za Mikoa kilichofanyika kwa siku 2 katika ukumbi wa Mtemi Isike Mwanakiyungi Mjini hapa.
Alisema tangu kuanzishwa kwake taasisi hiyo imefanya kazi kubwa kutekeleza miradi mbalimbali ya maji vijijini hali iliyopelekea kuongeza upatikanaji huduma hiyo kwa asilimia kubwa tofauti na hali ilivyokuwa huko nyuma.
Alibainisha kuwa RUWASA imetekeleza kwa kiwango kikubwa dhamira ya Rais Samia Suluhu Hassan ya kumtua ndoo mama kichwani, hivyo akawataka watendaji wake kuendeleza dhamira hiyo ili kupunguza zaidi kero ya maji vijijini.
Alitoa mfano wa utendaji kazi wa RUWASA katika Mkoa wa Tabora kuwa tangu kuanzishwa kwake miaka 4 iliyopita wamewezesha hali ya upatikanaji huduma ya maji safi na salama kufikia asilimia 62.9 kutoka asilimia 44 ya awali.
Alieleza kuwa miradi ipatayo 143 yenye thamani ya zaidi ya sh bil 44 imetekelezwa mkoani hapa ambapo miradi 113 ilitekelezwa na mafundi wa ndani (local fundi) na miradi 30 walipewa wakandarasi wa nje.
Balozi Batilda alishauri Wizara ya Maji kufanya tathmini ya utendaji wa RUWASA tangu kuanzisha kwake na hali ya upatikanaji huduma ya maji vijijini kwa sasa ikilinganisha na hali ilivyokuwa kabla ya kuanzishwa kwa wakala huo.
Alibainisha kuwa tathmini hiyo itasaidia kuweka mwelekeo mpya wa utoaji wa huduma ya maji vijijini chini ya Sheria ya Huduma za Maji na Usafi wa Mazingira namba 5. ya mwaka 2019 iliyoanzisha taasisi hiyo.
Naye Mkurugenzi Mkuu wa RUWASA, Clement Kivegalo alibainisha lengo la kikao kazi hicho kuwa ni kuwafanya wajumbe wa Sekretarieti za Mikoa yote nchini kuwa na uelewa wa pamoja kuhusu majukumu ya Wakala huo hivyo kuwasemea kwa uwazi mbele ya wananchi.
Alieleza kuwa msingi wa kuanzishwa taasisi hiyo ni kufikisha huduma ya maji safi salama kwa wakazi wa vijijini na kuhakikisha miradi ya maji yote inayotekelezwa katika maeneo hayo inakuwa endelevu ili kuwanufaisha wananchi.