Breaking

Monday, 1 August 2022

MAMA ADAIWA KUMUUA MWANAE WA MIAKA MITATU KWA KUMCHAPA FIMBO - KILIMANJARO

Picha haihusiani na tukio


Na Lango La Habari

Jeshi la Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, linamshikilia mwanamke mwenye miaka 27, Mkazi wa Kibosho Kirima Juu, Wilaya ya Moshi kwa tuhuma za kumuua mwanae mwenye umri wa miaka mitatu na miezi sita kwa kumchapa na fimbo.

Akithibitisha hilo mbele ya waandishi wa habari Kamanda wa Polisi Mkoani Kilimanjaro
ACP Simon Maigwa amesema tukio hilo limetokea jana Jumapili Julai 31, 2022 majira ya saa moja asubuhi.

Kamanda Maigwa amesema Mama huyo alimchapa na fimbo mwanae katika sehemu mbalimbali za mwili wake huku chanzo kikidaiwa kuwa mtoto huyo alifungulia bomba na kuchezea maji ya baridi yaliyokuwa yakitiririka.

" baada ya kuona hali ya mwanae imezidi kuwa mbaya mama huyo alijaribu kutoroka ila wananchi walimdhibiti na Jeshi la Polisi tulifanikiwa kumchukia kwa taratibu za kisheria" Amesema Kamanda Maigwa

Aidha Kamanda Maigwa ametoa wito kwa wazazi kutumia busara katika kuwaadhibu watoto wao pale wanapofanya kosa na sio kuchukua hatua kali hali inayopelekea kuhatarisha maisha.

"Kitendo cha kuchapa sio suluhisho kumfanya mtoto awe mtiifu, wazazi tumieni njia za busara, huyu mtoto alikuwa na miaka mitatu na miezi sita bado ni malaika haelewi chochote" amesisitiza Kamanda Maigwa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia langolahabari@gmail.com au WhatsaApp: +255 621 896 990

Pages