Breaking

Sunday, 7 August 2022

NAIBU WAZIRI MASANJA AFUNGA MAFUNZO YA KUKABILIANA NA USAFIRISHAJI HARAMU WA WANYAMAPORI




Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Mary Masanja (Mb) amefunga mafunzo ya siku tano ya kukabiliana na ujangili na usafirishaji haramu wa mazao ya wanyamapori na mimea ndani na nje ya Bara la Afrika uliofanyika leo jijini Dar es Salaam.

Akizungumza katika mafunzo hayo Mhe. Masanja amesema kuwa mafunzo hayo yametoa mbinu za kuhakikisha hifadhi zinahifadhiwa vizuri ili kulinda wanyamapori na kuendeleza utalii.

“Wataalamu wa masuala ya uchunguzi wamejifunza mbinu za kuzuia uharibifu wowote unaoweza kutokea kwenye maeneo ya hifadhi katika nchi wanachama wa Mkataba wa Lusaka (Lusaka Agreement)”.

Amesema mafunzo hayo yameshafanyika katika nchi za Tanzania, Kenya na Uganda na Tanzania itaendelea kushiriki kama nchi mwanachama ili kuzilinda hifadhi na wakati huohuo kuendeleza utalii.

Naye, Mkurugenzi Msaidizi wa Kuzuia Ujangili, Wizara ya Maliasili na Utalii, Bw.Robert Mande amesema kuwa mafunzo hayo yataendelea kufanyika ili kutekeleza sera za Serikali za kuendeleza uhifadhi.

“Lazima tuhakikishe kuwa tunalinda rasilimali za wanyamapori ili watalii wanavyokuja waweze kuziona na waweze kuwa na usalama”Mande amefafanua.

Ameongeza kuwa washiriki zaidi ya 21 kutoka nchi wanachama wamejengewa uwezo katika masuala ya uchunguzi, upelelezi, intelijensia na uendeshaji mashitaka ili waweze kufikia viwango vya umahiri mkubwa kwa sababu makosa ya ujangili yanavuka mipaka ya nchi na yanahitaji ushirikiano na vyombo vingine vya nje ya nchi.

Kwa upande wake Mshiriki wa Mafunzo kutoka nchini Kenya, Bw. Jami Yamina amesema mafunzo hayo yametoa mbinu mbalimbali za kutumia ili kuwakamata majangili na kuzikamata mali zao na kuziwasilisha mahakamani.

“Tukiweza kuwakamata hawa majangili tutakuwa tumefanikiwa kuzuia biashara hii haramu ya wanyamapori ” amesisitiza.

Mafunzo hayo yamehudhuriwa na wataalamu wanachama wa Lusaka Agreement (unaojihusisha na kuzuia uuzaji, usafirishaji wa wanyamapori pamoja na mimea) Grace Farm Foundation, US Homeland Security na washiriki kutoka nchini Uganda, Kenya na Tanzania.
Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia langolahabari@gmail.com au WhatsaApp: +255 621 896 990

Pages