Na Said Muhibu
Kocha wa klabu ya ligi kuu Uingereza (Premier league) Manchester United Eric Ten Hag ameonesha hali kutoridhishwa na kitendo cha Mshambuliaji wa kimataifa wa Ureno Christiano Ronaldo cha kutoka nje ya uwanja wakati mchezo wa kirafiki dhidi ya klabu ya ligi kuu Uhispania (La Liga) Rayo Vallecano ikiendelea kuchezwa siku ya Jumapili Julai 31, 2022.
Katika mchezo huo Ronaldo alicheza kipindi cha kwanza chote na akafanyiwa mabadiliko mwanzo wa kipindi cha pili, hapo ndipo alipochukua uamuzi wa kuondoka nyumbani kwake hali ya kuwa mchezo huo ukiendelea kuchezwa na kutamatika kwa sare ya 1-1.
Eric Ten Hag alionesha hali ya kutoridhishwa na kitendo hicho pale alipoulizwa na chombo cha habari cha Viaplay Sports Nchini Uholanzi juu ya kitendo cha Ronaldo kuondoka wakati mchezo huo ukiendelea.
"Hakika haikubaliki. Nimewaambia kwamba haikubaliki," alijibu swali aliloulizwa na chombo hicho cha habari.
"Sisi ni timu, sisi ni kikosi na unapaswa kubaki hadi mwisho,” aliongezea.
Kumekuwa na hali ya kutoridhishwa kwa Mshambuliaji wa Kimataifa wa Ureno Christiano Ronaldo juu ya mustakabali wake klabuni hapo na amekuwa akilazimisha kuachana na klabu hiyo kwasababu ya kutofanikiwa kufuzu kwenye mashindano ya klabu bingwa barani ulaya kwa msimu ujao huku Manchester United ikiendelea kusisitiza kuwa mchezaji huyo hauzwi.
Shirika la habari la The Sun liliripoti Ronaldo ana hati hati ya kuwekwa benchi kwa msimu ujao kutokana na kushindwa kushiriki mazoezi ya pamoja na wachezaji wenzake pamoja na kucheza michezo mingi ya kirafiki kwa kipindi alichokuwa Ureno kwasababu za kifamilia.
Eric Ten Hag anatarajia kuendelea kutumia mfumo wa washambuliaji watatu katika safu ya mbele akiwemo Marcus Rashford, Jadon Sancho na Anthony Martial ambapo imempa matokeo mazuri kwenye michezo yake yote ya kirafiki.
Ronaldo mwenye umri wa miaka 37 amebakisha miezi 12 tu kusalia na klabu ya Manchester United huku bado hatma yake ya kuendelea kuichezea klabu ya Manchester United bado haijafahamika.