Naibu Katibu Mkuu wa CCM Bara, Christina Mndeme (aliyesimama katikati) akizungumza na wajumbe wa halmashauri kuu ya CCM wilaya ya Kigoma Mjini alipofanya ziara ya kichama ya siku moja katika wilaya hiyo akiwa kwenye ziara mkoani Kigoma.
**********
CHAMA Cha ACT Wazalendo wilaya ya Kigoma Mjini kinatuhumiwa kupenyeza wanachama wake kugombea nafasi za uongozi kwenye uchaguzi wa ndani wa CCM kwenye ngazi za kata na matawi na wilaya ikidaiwa ni mpango wa chama hicho kunasa siri na mikakati ya CCM kuelekea uchaguzi mkuu wa mwaka 2025.
Mwenyekiti wa CCM wilaya ya Kigoma Mjini,Yassin Mtalikwa alibainisha hayo akitoa taarifa ya hali ya chama kwa Naibu Katibu Mkuu wa CCM Bara, Christina Mndeme anayefanya ziara mkoani Kigoma ambapo Mtalikwa amesema kuwa wamebaini njama hizo za ACT Wazalendo.
Mtalikwa alisema kuwa baada ya kubaini kuwepo kwa njama za wanachama wa ACT Wazalendo kujipenyeza kugombea nafasi za uongozi ndani ya CCM walichukua hatua kuhakikisha hakuna mgombea atakayepitishwa au kushinda kwenye chaguzi hizo ambaye siyo mwanachama halisi wa CCM.
Akizungumzia taarifa hiyo Naibu Katibu Mkuu wa CCM Taifa, Christina Mndeme amewataka viongozi na wanachama wa CCM kukataa kuwakumbatia mamluki wenye nia ya kudhoofisha juhudi za chama hicho hasa kwenye chaguzi na kuwataka kuwa kitu Kimoja.
Naibu Katibu Mkuu wa CCM bara alisema kuwa ni lazima viongozi na wanachama washikamane kuwa kitu kimoja na kupiga vita aina zote za njama zenye lengo la kuwadhoofisha ambapo ameonya vitendo vya kutolewa kwa siri za vikao na siri za chama hicho ni sumu kubwa kwa maendeleo ya chama.
“Hapa Kigoma kuna watu mchana wana kijani usiku wana nyekundu ni harati sana hiyo, hawa ni mamluki msiwape nafasi, shikamaneni muwe kitu kimoja na kuwapiga vita hawa mamluki,”Alisema Mndeme.
Alipoulizwa kuhusiana na tuhuma hizo Mwenyekiti wa ACT Wazalendo mkoa Kigoma, Ibrahim Sendwe alisema kuwa huko ni kutapatapa kwa baadhi ya wagombea ndani ya CCM ambao hawana uwezo kushindana na badala yake wanataka kubebwa na huruma za wajumbe.
Sendwe alisema kuwa wao kama chama kikubwa cha upinzani kusemwa kwenye vikao vya CCM ni lazima na kwamba katika hilo kuna dhamira ya baadhi ya viongozi kuwakata wagombea wao kwa madai ya usaliti lakini hilo linatokana na kwamba baadhi ya viongozi wanania ya kuwaengua wagombea wenye nguvu ambao siyo kambi yao kwa madai kwamba ni wapinzani au wasaliti.