TUKIO la kusikitisha limetokea Kilwa kufuatia mzee wa miaka 59 kujinyonga hadi kufa katika nyumba ya kulala wageni, Jeshi la Polisi limethibitisha kutokea kwa tukio hilo huku ushahidi ukieleza kuwa marehemu alikuwa na madeni mengi kutokana na kazi yake ya ufundi seremala.
Marehemu anafahamika kwa jina la Mshamu Omary Mpulu ambaye ni mkazi wa Tandika, Temeke Dar es Salaam anaripotiwa kuwa alifunga safari kuelekea Kilwa Somanga Wilaya ya Kilwa ambapo alichukua chumba katikanyumba ya wageni inaitwa Kinjumi iliyopo wilayani Kilwa.
Taarifa zinadai kuwa baada ya kulala na kufika asubuhi wahudumu wa nyumba hiyo ya wageni wakiwa na nia ya kufanya usafi waliona marehemu hatoki ndipo walipoamua kubomoa mlango walikuta marehemu amejinyonga kwa kujitundika dirishani kwa kutumia shuka ya nyumba ya kulala wageni.
Aidha Polisi wamebainisha kuwa mwili wa marehemu kwa sasa upo katika kituo cha afya cha Tingi kilichopo Wilayani Kilwa wakisubiriwa ndugu wa marehemu kwenda kuchukua mwili huo.
Kufuatia tukio hilo Jeshi la Polisi Mkoa wa Lindi limetoa wito kwa wananchi wote kutochukua maamuzi magumu ya kujinyonga hasa wanapokabiliwa na changamoto za kimaisha kwani changamoto zipo na wajitahidi kuhakikisha kuwa wanapambana nazo.