Breaking

Friday, 19 August 2022

WAZAZI KALIUA WALALAMIKIA WALIMU MAFATAKI



NA LUCAS RAPHAEL,TABORA

WAZAZI na walezi wilayani Kaliua Mkoani Tabora wamelalamikia tabia ya baadhi ya walimu kuwalaghai wanafunzi wao na kufanya nao mapenzi na kupelekea kupata mimba za utotoni.

Wametoa malalamiko hayo jana mbele ya Katibu wa Halmashauri Kuu ya CCM, Itikadi na Uenezi Shaka Hamdu Shaka aliyepo ziarani Mkoani hapa baada ya kuwapa nafasi ya kueleza kero zao.

Nixon Erasto (50) mkazi wa Kata ya Mwongozo katika Jimbo la Ulyankulu alilalamikia baadhi ya walimu wa shule ya sekondari Mwongozo kufanya mapenzi na wanafunzi wao na kuwapa mimba pasipo kuchukuliwa hatua yoyote.

Alisema walimu hao wamekuwa wakirudisha nyuma maendeleo ya watoto wa kike kwa kuwalaghai na kufanya nao mapenzi na kinachowasikitisha zaidi ni kuona walimu wanaofanya vitendo hivyo wakilindwa hata wanapotoa taarifa.

‘Juzi tu kuna mwalimu kakamatwa kwa kufanya mapenzi na mwanafunzi lakini akatoroka na hajakamatwa hadi leo, na siyo huyo pekee yake, kuna walimu wengi wenye tabia za namna hiyo, Kiongozi tunaomba utusaidie’, alisema.

Ngumba Rashidi (48) mkulima mkazi wa Ulyankulu alisema baadhi ya walimu hawana maadili mazuri, licha ya kuonywa kwa tabia hiyo bado wamekuwa wakiendeleza vitendo hivyo, hivyo akaomba hatua kali zichukuliwe.

Mkuu wa wilaya hiyo Paul Matiko Chacha alikiri kuwepo kwa baadhi ya walimu wenye tabia za namna hiyo ila akamhakikishia Katibu wa Itikadi na Uenezi kuwa tayari wameshachukua hatua stahiki kwa baadhi ya walimu.

Akizungumzia vitendo hivyo Shaka alimwagiza Mkuu wa Wilaya kuwasaka walimu wote wanaolalamikiwa kujihusisha na vitendo hivyo na wachukuliwe hatua kali za kinidhamu ili kukomesha tabia za namna hiyo.

Alisisitizia kuwa tabia za namna hiyo zinarudisha nyuma maendeleo ya mtoto wa kike kielimu hivyo kushindwa kufikia ndoto zao kimaisha, aliagiza Ofisi ya Mkuu wa wilaya na Mkurugezi wa halmashauri hiyo kumaliza tatizo hilo.

Kwa upande wake Katibu wa Jumuiya ya Wazazi Taifa Gilberth Kalima alisema ni kosa kisheria kumpa mimba mwanafunzi, yeyote anayebainika kufanya vitendo vya namna hiyo asiyefumbiwe mcho, akamatwe na kuchukuliwa hatua.

Alizitaka Kamati za Utekelezaji za Jumuiya ya Wazazi katika Mikoa yote kujadili na kuweka mikakati itakayosaidia kumaliza vitendo vya ukatili wa kingono wanavyofanyiwa watoto wa kike ili kuwawezesha kufikia ndoto zao.

Mwisho.
Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia langolahabari@gmail.com au WhatsaApp: +255 621 896 990

Pages