Na Mwandishi Wetu, Shinyanga
Serikali mkoani Shinyanga kwa kushirikiana na Jeshi la Polisi, wamefanikiwa kuzuia ndoa ya kimila iliyokuwa inahusisha Watoto, iliyokuwa ifanyike katika Kijiji cha Manyuda Kata ya Usanda, Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga.
Kwa Mujibu wa taarifa kutokea eneo la tukio, tukio hilo limetokea Jumanne Agosti 16, 2022 majira ya saa 12 jioni, baada ya Jeshi la Polisi Dawati la Jinsia kwa kushirikiana na Maafisa Maendeleo ya Jamii, kupata taarifa na kufika kwenye familia ambapo ndoa hiyo ilikuwa ikifungwa, na kukuta sherehe za ndoa zikiendelea.
Taarifa hiyo imesema kuwa, Bibi harusi katika ndoa hiyo ni mtoto mwenye umri wa miaka 15, ambaye inadaiwa kutolewa mahali ya Ng’ombe 10 na fedha taslimu kiasi cha shilingi laki mbili, ambapo angechukuliwa muda mfupi baada ya zawadi kutolewa na kwenda kuishi Maisha ya ndoa na Mume wake, (Bwana harusi) anayeishi katika kijiji kimoja kilichopo Wilayani Kishapu.
Hata hivyo wakati wa tukio hilo Bwana harusi ambaye hakukutwa katika eneo la tukio wakati wa zoezi la ukamataji, anadaiwa kuwa na umri wa miaka 17 .
Akifafanua juu ya tukio hilo, Afisa Maendeleo ya Jamii wa Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga Deus Mhoja, alisema walipokea taarifa za ndoa hiyo kutoka kwa raia wema na wao bila kuchelewa walitoa taarifa hizo Jeshi la Polisi, ambapo baada ya kufika eneo la tukio familia ya mtoto huyo walikuta sherehe za ndoa zikiendelea zikiwa zimefikia hatua ya utowaji wa zawadi kwa Bibi harusi.
Mhoja amesema wamechukua hatua hiyo kwa kuzingatia takwa la Sheria ya Mtoto ya Mwaka 2009 inayozuia ndoa kwa Watoto walio chini ya umri wa miaka 18.
Wakati huo huo, Jeshi la Polisi mkoani hapo limemkamata Mama mzazi wa mtoto huyo pamoja na mjomba wake aitwaye Festo Kisinza, kwa mahojiano zaidi na watafikishwa Mahakani baada ya upelelezi kukamilika.
Wakati wa zoezi hilo Baba mzazi wa binti huyo na ndugu wengine wa karibu, wakiwemo Wazazi wa upande wa Bwana harusi, hawakukutwa eneo la tukio kutoka na kile kilichoelezwa kuwa, walijificha baada ya kuhisi uwepo wa Polisi.
MWISHO