Kiwanda cha kuchenjua Madini ya Shaba kinatarajiwa kuanzishwa wilayani Tunduru Mkoa wa Ruvuma ili kuwezesha shughuli za kuchenjua madini hayo kufanyika nchini na hivyo kulinufaisha taifa na watanzania.
Hayo yamebainishwa na Waziri wa Madini, Dkt. Doto Biteko leo Agosti 16, 2022 mkoani Mwanza alipokutana na Kampuni ya Mineral Access System Tanzania Limited inayotarajia kujenga kiwanda cha kuchenjua madini ya Shaba katika eneo la Mbesa wilayani Tunduru.
Dkt. Biteko, amewapongeza kuwekeza nchini kwani uwepo wake utasaidia kuongeza thamani ya madini na hivyo kuongeza tija ya kiuchumi kwa taifa na kwa wanachi wa Tunduru.
Amesema, Serikali itaendelea kuvutia wawekezaji ili kuwekeza katika Sekta ya Madini kwa kuwa tayari imeweka mazingira wezeshi kwa wawekezaji kwenye mnyororo wote wa shughuli za madini ikiwemo shughuli za utafiti, uchimbaji na uongezaji thamani madini nchini bila changamoto yoyote.
"Serikali kupitia Wizara ya Madini itaendelea kuvutia wawekezaji kuja kuwekeza katika Sekta ya Madini ili Watanzania wanufaike na rasilimali hiyo," amesema Dkt. Biteko.
Vile vile, Dkt. Biteko amesema Serikali itahakikisha inaweka mazingira wezeshi ili kutatua changamoto ya ucheleweshwaji wa mizigo kuingia nchini kutokana na taratibu za forodha. Aidha amesisitiza kuwasilisha changamoto hiyo katika mamlaka husika.
Kwa upande wake, Rais na Mtendaji Mkuu wa Kampuni ya Metallica Commodities Corp, Glendon Archer amesema kiwanda hicho kitawezesha kuboresha maisha ya wananchi katika maeneo hayo na kuongeza Pato la Taifa.
Pia, ameahidi kushirikiana na Serikali katika kipindi chote cha uzalishaji ili manufaa ya kiwanda hicho yabaki nchini.
Archer amemshukuru Dkt. Biteko kwa ushirikiano anaopatiwa na Wizara ya Madini katika kila hatua ili kuweza kujenga kiwanda hicho na kuanza uzalishaji.
Kwa upande wake Mbunge wa Jimbo la Tunduru Kusini, Mhe. Daimu Mpakate, amesema kiwanda hicho kitaongeza fursa mbalimbali kwa wananchi na Serikali.
Ameongeza kuwa, wawekezaji hao wa madini ya Shaba watatoa ajira na kuboresha miundombinu ya maeneo hayo hususan kwa wakazi wa Tunduru.
Kampuni ya Mineral Access System Tanzania Limited pia inatarajiwa kuwekeza kwenye madini ya Lithium na Nikeli nchini.