Na Lucas Raphael ,Tabora
VIJANA wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania wameahidi kuwa mabalozi wa sensa kwa kutoa elimu kwa familia na jamii ili kuongeza uelewa na umuhimu wa kupata takwimu zinazohitajika katika mipango ya maendeleo endelevu ya taifa.
Akisoma risala ya kufunga kongamano hilo mbele ya askofu msaidizi wa kanisa la Dayosisi ya Magharibi kati Newton Maganga mwenyekiti wa vijana wa kanisa hilo Julian Kagambo alisema lengo la vijana ni kulisaidia kanisa na jamii .
Alisema kwamba vijana wanatambua umuhimu wa kuchangia maendeleo ya taifa kwa ujumla hivyo ni wajibu wa kila kijana kushirikia kikamilifu kufanikisha zoezi hilo
Kagambo alisema kwamba vijana na watanzania wote wanaitajika kujitokeza kuunga jitiada za serikali ili kuweza kutambua idadi ya wananchi wake ili iwe rahisi kuweza kupanga maendeleo.
Alisema tukio hilo la kitaifa ambalo linafanyika kila baada ya miaka 10 la kujua idadi ya watanzania kwa lengo la kupanga maendeleo ya watanzania wakiwemo vijana ambao ndio wanatakiwa kulisaidia taifa kutoa hamasa juu ya sensa.
Aidha Kagambo alisema kwamba vijana wanathamini kukua kwa utandawazi unaoendana na mabadiliko katika Maisha ikiwepo mmonyoko wa maadili, hivyo kanisa na taifa kwa ujuma liendelee kuwafundisha vijana kutumia utandawazi kwa akili, maarifa na kujali zaidi fursa zinazowanufaisha.
hata hivyo alisema kwamba wanatoa wito kwa taasisi za kidini na mashirika mbalimbali kutoa elimu ya malezi na makuzi kwa Watoto na vijana.
Alisema kwamba Wazazi na walezi wawe mstari wa mbele katika kufundisha Watoto na vijana misingi ya malezi bora, kwa kuwa kupungua kwa maadili na malezi ni chanzo cha uhalifu katika jamii.
Hata hivyo vijana wa Kanisa hilo walsema wao ni kielelezo cha Kanisa, hivyo wanaomba nafasi za uwakilishi wa vijana kwenye vyombo vya kimaamuzi na kiutendaji uwe kwa asilimia 20 kwa kuzingatia jinsi.
Kagambo alisema kwamba nafasi hizo za maamuzi ni kuanzia katika ngazi ya Mitaa, Sharika, Majimbo na Dayosisi na ngazi ya juu ya KKKT pamoja na uwakilishi katika Kamati mbalimbali ambazo huundwa mara kwa mara kwa ajili ya masuala maalumu yanayohusu kanisa.
mwisho