Watu 16 wamekamatwa Mkoani Mwanza kwa tuhuma za kuhujumu miundombinu ya Shirika la umeme Tanzania (Tanesco) na kusababisha hasara ya shilingi Milioni 18.
Watuhumiwa hao wamekamatwa katika operesheni ya siku nane iliyofanywa na Maafisa Usalama wa Tanesco Mkoa wa Mwanza kwa kushirikiana na Jeshi la Polisi kuanzia Agosti Mosi, 2022.
Akizungumzia kuhusu operesheni hiyo Afisa Usalama wa Tanesco, Jeverino Pembe amesema kuwa watuhumiwa hao 16 wamekamatwa katika maeneo ya Wilaya ya Magu,Nyamagana, Kwimba na Magu huku shirika likipata hasara ya jumla ya kiasi cha shilingi milioni 18.
Pembe amesema wizi wa miundombinu katika Shirika hilo umeweza kusababisha hasara kubwa na kurudisha nyuma juhudi za kuwahudumia wananchi.
Amewataka wananchi wenye tabia za wizi na uharibifu wa miundombinu ya Shirika hilo kuacha tabia hiyo ya kuiba nyaya za shaba katika transfoma hali inayohatarisha usalama na kuleta wakisababisha hasara kubwa.
Katika operesheni hiyo Maafisa Usalama wa Tanesco kanda ya ziwa,kwa kushirikiana na Jeshi la Polisi mkoani Mwanza wamefanikiwa kumkamata mfanyabiashara wa vyuma chakavu Bahati Stanley Kessy katika eneo la Igoma akiwa mmoja wa watuhumiwa wanaohujumu miundombinu ya umeme.