Na Lucas Raphael,Tabora
WAKANDARASI wazawa waliopewa kazi katika mradi mkubwa wa bomba la mafuta kutoka Hoima nchini Uganda kuja Chongoleani (Tanga) wametakiwa kufanya kazi kwa weledi ili serikali iendelee kuwaamini na kuwapa kazi nyingine.
Hayo yamebainishwa Julai 25, 2022 na Waziri wa Nishati January Makamba alipofanya ziara maalumu kutembelea eneo kinapojengwa kiwanda kikubwa cha kutengeneza mabomba yatakayotumika kusafirisha mafuta ghafi ya mradi huo.
Alisema kiwanda hicho kinachojengwa katika Kijiji cha Sojo, Kata ya Igusule, wilayani Nzega Mkoani hapa kinatakiwa kukamilika haraka kwa ubora na weledi unaotakiwa ili kazi ianze kutokana na umuhimu wake kwa uchumi wa taifa.
Alibainisha kuwa makampuni ya ndani yanaposhiriki katika miradi mikubwa kama hiyo wanapata uzoefu na nchi inapata manufaa lakini wanapofanya vibaya au kuchelewesha kazi wanakwamisha juhudi za serikali na kutokuaminika.
‘Miradi huu una manufaa makubwa kwa serikali, hivyo wakandarasi wa ndani wanaposhirikishwa wanapaswa kufanya kazi kwa weledi na viwango ili iwe rahisi kupata kazi nyingine zinazotekelezwa hapa nchini’, alisema.
Waziri Makamba aliongeza kuwa matarajio ya serikali ni mradi huo kuanza kazi ifikapo mwishoni mwa mwaka huu hivyo akaagiza kila mkandarasi aliyepewa kazi katika mradi huo kutimiza wajibu wake ipasavyo.
Alizitaka kampuni zote kushirikiana ili kuharakisha utekelezaji wake, alitaja baadhi ya kampuni hizo kuwa ni Milembe Construction Company Ltd (ya wazawa), ECOP (East African Crude Oil Pipe line) na ISOAF ambao wamepewa kazi ya kutengeneza kiwanda hicho.
Mbunge wa Jimbo la Bukene Seleman Zedi ambapo mradi huo upo, aliishukuru serikali kwa kuleta mradi huo katika kijiji hicho na kuwapelekea umeme wa uhakika katika eneo hilo, sasa wananchi wameanza kunufaika kwa kupata ajira.
Aliongeza kuwa serikali pia imewapatia kiasi cha sh mil 500 kwa ajili ya ujenzi wa kituo cha afya katika kata hiyo ili kuboresha huduma za afya kutokana na muingiliano wa watu wengi aidha alisema halmashauri pia inatarajia kupata tozo ya huduma kiasi cha sh bil 1.8 kutokana na mradi huo.
Mkuu wa Mkoa huo Balozi Dkt Batilda Burian alisisitiza kuwa dhamira yao ni kuona mradi huo ukiwanufaisha wakazi wa Mkoa huo katika nyanja zote ikiwemo ajira, kupata fursa ya kutoa huduma za chakula, ulinzi na mengineyo.
Mwisho