Breaking

Wednesday, 20 July 2022

WAZIRI MKUU AKIPONGEZA CHUO CHA OPEN UNIVERSITY, AMPATIA AJIRA MWANAFUNZI BERNADETHA



Na Mwandishi wetu, Dar es Salaam

Waziri Mkuu wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Kassim Majaliwa amekipongeza Chuo Kikuu Huria cha Tanzania (Open University) kupitia kitengo cha teknolojia kwa kusaidia wanafunzi wenye mahitaji maalumu kufikia malengo yao ambayo wanatarajia.

Pongezi hizo amezitoa jijini Dar es Salaam wakati wa ufunguzi wa maonesho ya 17 ya Elimu ya Juu, Sayansi na Teknolojia yanayo ratibiwa na kusimamiwa na Tume za Vyuo Vikuu Nchini (TCU) wakati alipotembelea Banda la Chuo hicho na kukutana na Mwanafunzi aliyeandika kitabu cha kipenga Cha mwisho licha ya kuwa na uono hafifu.

Waziri Majaliwa amevutiwa sana na namna Mwanafunzi huyo alivyoweza kuandika kitabu chake ambacho kinatoa motisha kwa watu kutokukata tamaa hata kama wanapitia changamoto gani wanatakiwa kupambana.

Hata hivyo, Waziri Majaliwa ameweza kushuhudia namna Bernadetha anavyoweza kutumia vifaa vya teknolojia kwa ufanisi mkubwa katika kufanya kazi zake hivyo ameagiza zichukuliwe taarifa zake kwa ajili ya kuweza kupatiwa ajira na Tamisemi.

Kwa upande wake, Bernadetha Msigwa ambae ni Mwanafunzi wa Chuo hicho, amesema tatizo la kuwa na uono hafifu alilipata akiwa kati kati ya safari yake ya masomo lakini hakukata tamaa ameamua kujiendeleza na masomo kwani anaamini uwezo wa kufanya kazi anao.

"Nimeandika kitabu changu mwenyewe kwa kutumia Teknolojia ambayo nimejifunza Chuo Kikuu huria, kitabu changu kinaitwa kipenga Cha mwisho hii ikiwa na maana hutakiwi kukata tamaa ukiwa katika safari ya maisha unatakiwa upambane mpaka mwisho kwa sababu kila kitu kinawezekana"amesema Bernadetha.

Aidha, ameishauri Serikali kuongeza Teknolojia ya kujifunza kwa watu wenye uoni hafifu Ili watu wengi wenye matatizo hayo waweze kuipata na kutimiza ndoto zao.

Maoneaho ya 17 ya Elimu ya Juu,Sayansi na Teknolojia yanayo ratibiwa na kusimamiwa na Tume za Vyuo Vikuu Nchini (TCU) yamefunguliwa Julai 19 na Waziri Mkuu wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Kassim Majaliwa ambapo yatahitimishwa Julai 23 mwaka huu ambapo vyuo zaidi ya 53 vya elimu ya juu vimeshiriki katika maonesho hayo.
Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia langolahabari@gmail.com au WhatsaApp: +255 621 896 990

Pages