Breaking

Monday, 25 July 2022

WAZIRI BASHUNGWA AAGIZA WABADHIRIFU, WAZEMBE HALMASHAURI ZOTE KUCHUKULIWA HATUA



Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Innocent Bashungwa amemuagiza Mkuu wa Mkoa wa Morogoro (RC), Martin Shigela kuwachukulia hatua wote waliotajwa na timu maalumu iliyochunguza mifumo ya ukusanyaji mapato katika Halmashauri ya Kilosa.

Pia, amewaagiza wakuu wa mikoa wote nchini kutekeleza maelekezo ya Mdhibiti na Mkaguzi wa Hesabu za Serikali (CAG) na kuwashughulikia waliotajwa kwenye ripoti katika muda uliotolewa.

Taarifa iliyotolewa na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini-Tamisemi leo Jumatatu Julai 25, 2022 imesema, Bashungwa ametoa maagizo hayo wakati akizungumza na watumishi wa Halmashauri ya Kilosa baada ya kupokea ripoti ya uchunguzi iliyofanywa katika Halmashauri hiyo Machi, 2022.

“Si wakati sasa wa kubebana wala kuoneana aibu, hatumtendei haki Rais Samia Suluhu Hassan, pale inapokuja miradi wanatokea watu wachache wanaenda tofauti na taratibu za utumishi wa umma, ninachotaka sasa kila Mkuu wa Mkoa achukue hatua kwenye eneo lake,” amesema Waziri Bashungwa

"Sisi watumishi wa umma tulioaminiwa na Watanzania ndani ya Serikali lazima tuendelee kuwa waaminifu, waadilifu na maelekezo hayo Rais amekuwa akiyasema mara nyingi. Kwa watumishi ambao mko Tamisemi tutaendelea kuchukua hatua bila kuchoka mpaka tutakapobadilika," amesema

Amesema taarifa ya timu maalumu ya uchunguzi uliofanyika kilosa imebaini kuwepo matumizi mabaya ya mashine za kieletroniki za ukusanyaji mapato (POS) huku baadhi ya watumishi wakishirikiana na wakusanya mapato kuhujumu mashine hizi.

"Kwa madudu yaliyobainika hapa Mwenyekiti wa Halmashauri, Baraza la Madiwani na Kamati ya Fedha na uongozi inabidi kubadilika, na hii ni kwa Kamati za fedha na uongozi ndani ya halmashauri zetu zote zinapaswa kujitafakari," amesema

Amesema uchunguzi ulibaini kati ya POS 239, POS 12 hazijulikani zilipo na hakuna taarifa ya upotevu, POS mbili zilipotea lakini vielelezo vyake havijapatikana, POS zote 239 kutokua na namba za utambuzi pamoja na watumiaji wote wa POS kutumia nywila inayofanana.

Pia imebainika upungufu katika kunakili taarifa za POS kwenye rejista, wakusanya mapato kutochukua asilimia sita kama fedha za malipo yao kama mkataba unavyoeleza na uwepo wa Leseni za biashara 1,630 zilizoisha muda wa matumizi bila kuhuishwa tangu mwaka 2017 hadi Machi 2, mwaka huu hali ambayo imeifanya halmashauri kupoteza Sh335.3 milioni.

Bashungwa amesema uchunguzi huo pia umebaini fedha ambazo hazikupelekwa benki ni Sh680 milioni na wakusanya mapato kutokuwa na mikataba ya kukusanya mapato na miamala iliyorekebishwa yenye takribani Sh4.1 bilioni bila kuzingatia taratibu kutokana na udhaifu wa ndani katika Idara ya Fedha.

"Fedha hizi zote zingekusanywa na kuelekezwa kwenye shughuli za maendeleo zingeleta tija, lakini kuna watu wachache wanawachelewesha na kudhulumu haki ya wananchi ambayo Rais anaitekeleza, hatutawavumilia," amesema

"Haya mambo yasiwacheleweshee maendeleo wananchi wa Kilosa, kuna watu mchwa ndani ya halmashauri tutaendelea ku-deal (kuwashughulikia) na kama kuna wengine kwenye halmashauri zingine wembe ni huu."

"Mkuu wa Mkoa wa Morogoro jipange, tumia vyombo vyako vya ulinzi kuwashughulikia yeyote ambaye anachezea mifumo ya ukusanyaji wa mapato na anafanya ubadhirifu kwenye fedha za Serikali, sheria zipo zinaruhusu.”




“Endelea kudhibiti matumizi ya fedha kutoka Serikali Kuu na fedha za mapato ya ndani hakikisha zinaelekezwa kwenye utekelezaji wa miradi katika Kata tena miradi yenye tija,” amesema

Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Shigela amesema atatekeleza maelekezo yote yaliyotolewa na Waziri Bashungwa.

Pia, Shigela amesema wamewekwa mkakati wa kudhibiti mianya ya upotevu mapato, kutozalisha madeni mapya na kuwabainisha wanaodaiwa miaka ya nyuma ili wafikishwe kwenye vyombo vya sheria.
Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia langolahabari@gmail.com au WhatsaApp: +255 621 896 990

Pages