Breaking

Sunday, 24 July 2022

WAZIRI BASHUNGWA AAGIZA KUCHUNGUZWA UBADHIRIFU WA FEDHA SHULE YA PROF. KABUDI



Na OR- TAMISEMI

Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Mhe. Innocent Bashungwa ameagiza timu ya uchunguzi kutoka Ofisi ya Rais TAMISEMI kufika Halmashauri ya Wilaya ya Kilosa kuchunguza thamani ya fedha katika ujenzi wa shule mpya ya Sekondari ambayo wananchi wamependa iitwe Prof. Kabudi.

Mhe. Bashungwa ameagiza hayo mapema leo Julai 23 mwaka 2022 wakati wa ziara yake wilayani humo kukagua utekelezaji wa miradi ya maendeleo na kuzungumza na wananchi.

Amesema shule hiyo ni miongoni mwa shule 15 zilizopata Sh bilioni 1 kwa ajili ya kujenga shule ya Sekondari za Kidato cha Tano na Sita kupitia mradi wa Lipa Kulingana na Matokeo(EP4R).

' Shule za maeneo mengine zilizopata fedha kama hizo zimekamilisha ujenzi lakini katika shule hii ni tofauti shule haijakamilika na fedha zimeisha.

" Pia gharama za ujenzi zimekua juu sana kuanzia kwenye ujenzi madarasa, mabweni, nyumba za walimu hazijakamilika sasa nataka timu maalum ije kuangalia thamani ya fedha zilizotumika."


Aidha, Bashungwa amemuagiza Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Martin Shigela kuhakikisha anasimamia mapungufu yote yaliyobainika kwenye shule hiyo ili iweze kukamilika kwa ubora na kuanza kutumika.

Pia ameagiza shule hiyo ianze kutumika Mwezi September,2022 ili wanafunzi wa maeneo ya jirani waanze kunufaika na matunda ya Serikali yao.

" Anzeni sasa maandalizi ya kuwapangia wanafunzi, tunataka Septemba mpokee wanafunzi wa kidato cha tano na kuhamishia wanafunzi wa kidato cha kwanza."

Bashungwa amemuagiza Mkurugenzi wa Elimu ya Sekondari kutoka Ofisi ya Rais TAMISEMI, kuanza mara moja mchakato wa kuisajili shule hiyo.


Naye Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Mhe. Martine Shigela amesema kuwa Timu yake itakua shuleni hapo kuanzia Jumatatu ya Julai 25 mwaka huu kuanza uchunguzi katika ujenzi wa shule hiyo.

" Tulishakuja kukagua maendeleo ya ujenzi na kubaini kasoro, hivyo nikuhakikishie timu ya kuchunguza itaanza kazi jumatatu na itafanya kazi yake kwa umakini na haraka."

Alisema timu hiyo itaundwa na wataalam kutoka Wakala wa Majengo Tanzania(TBA), Shirika la Nyumba la Taifa na TAMISEMI.
Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia langolahabari@gmail.com au WhatsaApp: +255 621 896 990

Pages