Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo. Mhe, Mohamed Mchengerwa amesema watu zaidi ya milioni kumi wameshuhudia matembezi ya kiutamaduni katika jiji la Dar es Salaam.
Mhe. Mchengerwa ameyasema haya wakati akimkaribisha Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano kwenye uzinduzi wa tamasha la kwanza la kitaifa la Utamaduni jijini Dar es Salaam ambapo amefafanua kuwa idadi hiyo inatokana na watu walioshiriki moja kwa moja na wale walioangalia kupitia vyombo mbalimbali vya habari.
Amesema kufanyika kwa tamasha hili la kwanza la kitaifa la utamaduni ambalo limejumuisha matembezi ya kiutamaduni ni maono ya Mhe.Rais ya kutaka kukutanisha utamaduni wetu.
Ameongeza kuwa upekee wa tamasha hili ni kuwa limeandaliwa mahususi kwenye maadhimisho ya kilele cha siku ya kiswahili duniani.
Aidha, amefafanua kuwa Taifa lisilo na mila na desturi ni sawa na taifa lililo mateka na mufu.
Amemthibitishia, Mhe. Majaliwa, kuwa maelekezo aliyoyatoa kuhusiana na kuwa na mavazi ya taifa anakwenda kuyatekeleza mara moja.
Amesema Machifu takribani 50 wameshiriki katika tamasha hili ambapo amesisitiza kuwa Serikali itaendelea kuwaheshim na kuwatetea Viongozi hao wa kimila.
Aidha amewashukuru machifu kujitoa kwenye shughuli mbalimbali za Serikali hususan zoezi la kitaifa la sensa litakalifanyika Agosti 23, 2022.
Amesema tamasha hili ni la kipekee kwa kuwa limeshirikisha takribani mikoa yote ya Tanzania na limeshirikisha Utamaduni Carnival, usiku wa taarabu ambao utafanyika kwenye ufukwe wa Coco jijini Dar es Salaam Julai 3, 2022.
Ametoa wito kwa watu wengi kujitokeza kwa wingi kwenye usiku wa taarabu kwa kuwa hakuna kiingilio.