Watu watano wamefariki dunia na wengine kadhaa wamejeruhiwa baada ya lori la mizigo lililobeba shehena ya mahindi kufeli breki na kugonga badi dogo la abiria aina ya Coaster liliyokuwa likitoka Mbeya mjini kwenda Wilaya ya Mbarali.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, Urlich Matei amesema kuwa ajali hiyo imetokea Jumanne Julai 5, 2022 majira ya saa kumi jioni kwenye mteremko mkali wa barabara kuu ya Mbeya-Dar es Salaam
Kamanda Matei amesema kuwa lori la mizigo lililokuwa tela liligonga gari la abiria na kisha kuliburuza mpaka kwenye vibanda vilivyopo pembezoni mwa barabara na kusababisha vifo hivyo na majeruhi.
''Gari lililosababisha ajali lilitokea Mkoa wa Songwe kwenda jijini Dar es Salaam huku likiwa limebeba shehena za mahindi na chanzo cha ajali ni kufeli breki kutokana na mteremko mkali ambao alishindwa kulimudu'' amesema
Matei amesema miili ya watu waliofariki kwenye ajali hiyo imehifadhiwa kwenye kituo cha afya cha Inyala huku majeruhi wakipelekwa Hosptali ya Wilaya ya Igawilo ya Mbeya ambapo idadi yao bado haijafahamika.
Kamanda Matei amesema kuwa hiyo ni ajali ya pili kutokea kwenye eneo hilo kwa siku za hivi karibuni, ambapo June mwaka huu magari manne yaligongana huku mawili yakiteketea kwa moto na kusababisha kifo cha mtu mmoja.ADVERTISEMENT
Amesema kuwa kutokana na matukio hayo amewasiliana na Wakala ya Barabara Tanzania (Tanroads) kuona namna ya kuboresha njia ya mchepuko kutokana na magari mengi kufeli breki na kusababisha ajali kwenye mteremko huo.
Mkuu wa Wilaya ya Mbeya, Dk Rashid Chuachua amesema amemuagiza Mkuu wa Polisi Wilaya (OCD) kufika eneo la tukio na kutoa taarifa za vifo na hali za majeruhi.
Source: Mwananchi