Breaking

Monday, 18 July 2022

WATU SITA WAKAMATWA KWA TUHUMA ZA KUVUNJA MAJENGO NA WIZI WA MAGARI




Jeshi la Polisi Mkoa wa Mjini Magharibi Unguja limefanikiwa kuwakamata watuhumiwa sita wanaojihusisha na matukio mbalimbali ya kuvunja majengo pamoja na kuiba vifaa vya magari.

Kupita taarifa iliyotolewa na Jeshi la Polisi imeeleza kuwa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mjini Magharibi ACP Richard Tadei Mchomvu akizungumza na waandishi wa habari huko ofisini Madema, amesema watuhumiwa hao wamekamatwa tarehe 12 Julai 2022 huko wilaya ya Magharibi baada ya kufanyika kwa operesheni maalumu ya kupambana na vitendo hivyo.

"Tumewakamata watuhumiwa sugu sita ambao wako katika makundi mawili ambapo watatu ni wale wanaojihulisha na kuiba vifaa ambao ni Ibrahim Muhammad Sharif, miaka 19, mshirazi wa Magogoni, Juma Issa Victor, Miaka 22, mmakonde wa Magogoni na Ali Suleiman Mussa, miaka 20, mruguru wa Magogoni."

Aidha kamanda Richard amewataja watuhumiwa wengine wanaojihusisha kupokea na kununua mali hizo za wizi ambao ni Juma Mohamed Sinani, miaka 39, mshirazi wa Amani Freshi, Ibrahim Haji Kinange, miaka 26 , mshirazi wa Magomeni na Hilmi Suleiman Ali, miaka 22, Albsaid wa Nyarugusu.

Amesema wamekamatwa wakiwa na betri za gari 5 pamoja na mbao 15 zenye urefu tofauti ambazo baadhi ya vitu hivyo vimetambuliwa na wamiliki.

Hata hivyo Kamanda Mchomvu amesema watuhumiwa hao wanaendelea kuhojiwa na upelelezi utakapokamilika watafikishwa mahakamani.


Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia langolahabari@gmail.com au WhatsaApp: +255 621 896 990

Pages