Na Said Muhibu
Watu 20 kutoka wilaya nane katika eneo la Bihar Mashariki mwa India wamefariki dunia baada ya kupigwa na radi katika wilaya nane katika saa 48 zilizopita.
Waziri mkuu wa Bihar Nitish Kumar alionyesha masikitiko yake juu ya vifo kutokana na radi kati ya Jumatatu jioni na Jumanne.
Kumar amewaasa wananchi wa eneo hilo kufuata ushauri wanaopewa na Mamlaka ya usimamizi wa Maafa nchini juu ya kujikinga na majanga hayo.
Taarifa iliyotolewa na gazeti la The Times nchini India imesema Waziri Kumar alifanya mkutano na maafisa wa serikali juu ya uwekaji wa vizuia radi kwenye majengo yote ya serikali ikiwa ni pamoja na shule na hospitali.
Eneo la Bihar limekuwa likiripotiwa matukio ya wakazi wake kupigwa na radi mara kwa mara kutokana na miundombinu yake kuruhusu kushambuliwa na radi wakati wa mvua za masika.
Hata hivyo India Shirika la habari la BBC limeripoti India kuwa na matukio kama hayo mara kwa mara, huku kila mwaka mamia ya watu hufariki dunia kwa kushambuliwa na radi nchini humo.
India ilirekodi zaidi ya mapigo milioni 18 ya radi kati ya Aprili 2020 na Machi 2021, kulingana na utafiti wa Baraza la Matangazo la Mifumo ya Kustahimili Hali ya Hewa. Hili lilikuwa ni ongezeko la 34% katika kipindi kama hicho kwa mwaka uliopita.