Breaking

Saturday, 9 July 2022

WATU 10 WAUAWA WAKIWA ZAHANATI




Washambuliaji wamewauwa takriban wagonjwa kumi katika shambulio dhidi ya kliniki moja mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.

Waasi wanaoaminika kuwa wa kundi la Allied Democratic Forces (ADF), kundi lenye silaha la Uganda ambalo limekuwa likiendesha shughuli zake katika misitu minene ya mashariki mwa DRC kwa miongo kadhaa, walishambulia zahanati ya kanisa mwendo wa saa 10:00 usiku wa Alhamisi, mashahidi walisema Ijumaa.

Msemaji wa jeshi amethibitisha kutokea kwa shambulio hilo katika mji wa Lume katika jimbo la Kivu Kaskazini, lakini hakusema ni watu wangapi waliofariki.

Shahidi alisema kulikuwa na watu saba waliokufa, wakati muuguzi katika hospitali hiyo alisema idadi ya muda ni 13 na wengi bado hawajapatikana.

"Walimchoma baba yangu, Katika wodi ya hospitali kulikuwa na wagonjwa wanne ambao wote waliungua hadi kufa, katika kitengo cha watoto magodoro yote yamechomwa na katika wodi za pembeni tuliokota maiti tisa,” alisema Kule Mwenge Salomon, muuguzi wa kituo cha afya cha Lume.

Kakule Vikere Lem alikuwa akimlisha babake kwenye zahanati alipoona safu ya watu wakiwa na mienge wakikaribia mji, karibu kilomita 40 kusini mashariki mwa jiji la Beni.

"Nilikimbia, nikidhani kwamba wangeokoa hospitali, lakini kwa bahati mbaya walimchoma baba yangu hospitalini," Vikere alisema.

Uganda imetuma takriban wanajeshi 1,700 katika nchi jirani ya Kongo kusaidia kupambana na ADF baada ya kushutumu kundi hilo kuhusika na mashambulizi ya mabomu mjini Kampala mwaka jana.

ADF iliua zaidi ya watu 1,300 katika mwaka uliopita, wengi wao wakiwa katika mashambulizi ya usiku kwenye vijiji vya mbali, walisema wataalam wa Umoja wa Mataifa.
Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia langolahabari@gmail.com au WhatsaApp: +255 621 896 990

Pages