Breaking

Wednesday, 6 July 2022

WATATU WAHUKUMIWA KUNYOGWA, MAUAJI YA BODABODA - NJOMBE




Mahakama Kuu Kanda ya Iringa iliyokaa kikao chake katika mahakama ya hakimu mkazi mkoa wa Njombe imewahukumu washtakiwa watatu Elias Jackson Mwenda (31), Hussein Khamis (31) na Orestus Mbawala (51) kunyongwa hadi kufa baada ya kukutwa na hatia ya mauaji ya James Kaengesa mkazi wa Makambako mkoani hapa.

Akisoma hukumu hiyo jana Julai 6, 2022 Jaji Dk John Utamwa amesema tukio hilo la mauaji lilitokea mtaa wa Mashujaa uliopo halmashauri ya mji wa Makambako.

Amesema tukio hilo lilitokea Juni 2016 mnamo saa mbili usiku ambapo marehemu ambaye alikuwa dereva wa bodaboda aliyokuwa akiimiliki, alikodiwa na moja ya washtakiwa hao na alipofika eneo la Mashujaa aliambiwa asimame na mshtakiwa huyo ambaye alikuwa amepakiwa kwenye bodaboda hiyo.

Amesema eneo ambalo marehemu alisimamisha pikipiki yake hiyo kumbe washtakiwa walikubaliana endapo mwenzao atakodi bodaboda mpya asimame eneo hilo.

"Ndipo walimkaba marehemu na kumnyonga kwa kutumia kamba na kupora pikipiki," amesema Dk Utamwa.

Amesema baada ya kumyonga marehemu na kumuua washtakiwa hao walimtupa kwenye shamba la mahindi na kutoweka na pikipiki kuelekea mkoani Mbeya ambako walikamatwa eneo la Rujewa wakiwa na pikipiki hiyo.

Amesema hukumu hiyo kwa washtakiwa hao imetolewa kutokana na wao kwenda kinyume cha sheria chini ya kifungu cha 196 na 197 cha kanuni ya adhabu sura ya 16 marejeo ya mwaka 2019.

Awali mawakili wa Jamhuri, Matiku Nyangero na Andrew Mandwa waliiomba mahakama kutoa adhabu kwa mujibu wa kifungu cha 197 cha kanuni ya adhabu sura ya 16 marejeo ya 2019 kwa kuwa adhabu ya mauaji ya kukusudia ni moja tu ya kunyongwa hadi kufa.

"Pikipiki iliyokuwa kielelezo cha sita upande wa jamhuri iliyokuwa mali ya marehemu arudishiwe mke wa marehemu anayeitwa Enelika Nyenzi," amesema Nyangero.

Upande wa utetezi uliowakilishwa na Musa Mhagama, Byton Kaguo na Octavian Mbungani wamekubaliana na maombi yaliyotolewa na mawakili upande wa serikali.



Source: Mwananchi
Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia langolahabari@gmail.com au WhatsaApp: +255 621 896 990

Pages