Breaking

Tuesday, 5 July 2022

WANAUSHIRIKA WATAKIWA KUONGEZA THAMANI YA MAZAO



Na Lucas Raphael,Tabora

SHIRIKISHO la Vyama vya Ushirika nchini limetakiwa kuhamasisha wanaushirika kuzalisha bidhaa zenye ubora ili kuongeza thamani ya mazao yao na kunufaika na bei nzuri ya soko.

Hayo yamebainishwa juzi na Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Nzega Mjini alipokuwa akihitimisha kilele cha maadhimisho ya Siku ya Ushirika Duniani yaliyofanyika Kitaifa kuanzia Juni 28 hadi Julai 2, 2022 katika Viwanja vya Nane Nane, Ipuli Mjini Tabora.

Alisema dhamira ya serikali ya awamu ya 6 ni kuinua sekta ya kilimo ili kuongeza kasi ya uzalishaji ikiwemo kupanua wigo wa masoko, hivyo akataka wadau waliopewa dhamana ya kusaidia wakulima kutekeleza wajibu wao ipasavyo.

Alibainisha kuwa ushirika ni mfumo sahihi unaolenga kumsaidia mkulima kuboresha shughuli zake ili ziweze kumnufaisha na sio kuneemesha watu wachache kupitia jasho lao.

Ili kuhakikisha ushirika unakuwa na manufaa makubwa kwa wakulima aliwataka kuchagua viongozi wenye sifa na sio wanaotanguliza maslahi binafsi na kuwanyonya.

‘Yeyote anayetaka kujinufaisha kupitia jasho la mkulima hatutamfumbia macho, na kuanzia sasa ni marufuku vyama vya msingi kuwalipa Wahasibu wa Shirika la Ukaguzi wa Vyama vya Ushirika (COASCO) wanaokuja kuwakagua, chama kitakachowalipa tutafukuza viongozi wote’, alisema.

Waziri Bashe alifafanua kuwa katika bajeti ya mwaka huu serikali imetenga kiasi cha sh bil 150 kwa ajili ya ruzuku ya mbolea itakayotolewa kwa mikoa yote ili msimu mpya wa kilimo unapoanza wakulima wasihangaike.

Aidha aliongeza kuwa serikali itatoa ruzuku ya tani 5000 ya mbegu za alizeti kwa wakulima bure katika msimu ujao wa kilimo huku akibainisha zoezi la ugawaji mbegu hizo litakuwa endelevu hadi mwaka 2025.

Aliweka wazi kuwa serikali ya awamu ya 6 imeanza kufufua viwanda vyote vya kuchakata mazao ya wakulima (ginery) ikiwemo cha KACU na Manonga katika Mikoa ya Shinyanga na Tabora na kuagiza vyama vya ushirika vilivyokufa vifufuliwe.

Aidha Waziri Bashe alitoa fursa kwa wakulima kuuza mazao yao mahali popote penye soko na kuongeza kuwa serikali haitawafungia mipaka bali na kubainisha kuwa hakuna sababu ya kusubiri mnunuzi fulani wakati wapo wengine wenye fedha zao, alisisitiza kuwa kuanzia sasa hakuna kukopa mazao ya wakulima.

Mwisho.
Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia langolahabari@gmail.com au WhatsaApp: +255 621 896 990

Pages