Wachimbaji wadogo watatu wamefariki dunia na wengine wawili wamejeruhiwa baada ya kufukiwa na kifusi cha udongo wakati wa kichimba madini ya dhahabu katika machimbo ya Nyamatagata wilayani Geita mkoani Geita.
Akizungumza na Mwananchi Ijumaa Julai 15, 2022, Mkuu wa Wilaya ya Geita, Wilson Shimo amesema ajali hiyo imetokea jana.
Shimo amesema miili ya watu hao tayari imeopolewa na imehifadhiwa katika hospitali ya Mkoa wa Geita na majeruhi wanaendelea na matibabu katika hospitali hiyo.
Mkuu huyo wa wilaya amesema chanzo cha ajali hiyo ni wasimamizi wa mgodi kutokuwa makini na kuruhusu wachimbaji wadogo kuingia kwenye mashimo yasiyo imara.
“Kutokana na uzembe walioufanya tunawashikilia wasimamizi na wamiliki wawili wa leseni katika mgodi huo”
Kamati ya ulinzi na usalama ya wilaya imetembelea eneo hilo na kusitisha shughuli za uchimbaji hadi pale wamiliki watakaporekebisha mashimo hayo na kukaguliwa kama yanakidhi wachimbaji wadogo kufanya kazi.
Source: Mwananchi