


**********************
Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni UNESCO, kupitia programu yake ya “Our rights, Our Lives, Our future Plus” inayofahamika kama O3 Plus imeikabidhi Serikali nakala 800 za madaftari ya kusajili taarifa za ukatili wa kijinsia.
UNESCO imekabidhi madaftari hayo kwa Wizara ya Maendeleo ya Jamii Jinsia Wanawake na Makundi maalum katika uzinduzi wa dawati la jinsia la chuo kikuu cha Dodoma (UDOM) Julai 23, 2022.
Lengo la kukabidhi madaftari hayo ni kusajili na kutunza kumbukumbu za taarifa za vitendo vya ukatili wa kijinsia vinavyotolewa katika Dawati la Jinsia chuoni hapo.
Kwa kupitia mradi wa O3 Plus unaofadhiliwa na serikali ya Sweden UNESCO imechapisha nakala hizo za madaftari ya kusajili ikiwa na lengo la kuwezesha ufuatiliaji wa mwenendo wa shauri lililopewa rufaa, Kusaidia kuongeza wigo wa kupata taarifa za vitendo vya ukatili.
Pia Kuwezesha uandaaji wa taarifa za vitendo vya ukatili wa kijinsia zilizoripotiwa katika Dawati.
Aidha UNESCO inalenga kuongeza uelewa wa wadau zaidi ya 50,000 wa vyuo vikuu kuhusu ukatili wa kijinsia na vitendo vya unyanyasaji wa kingono, kutoa samani za ofisi kwa ofisi za madawati 10 ya jinsia ya vyuo vikuu, kutoa mafunzo kwa waratibu wa madawati ya jinsia wapatao 200 kutoka vyuo vikuu 15, na kuwezesha usambazaji wa nakala za vitabu vya rejista ya dawati la jinsia kwa mradi wote wa vyuo vikuu nufaika.