Breaking

Monday, 4 July 2022

TAMISEMI YAWAPA MAAGIZO WAKUU WA MIKOA NA WILAYA



Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa Serikali za Mitaa, Mhe. Innocent Bashungwa amewaagiza Wakuu wa Mikoa na Wakuu wa Wilaya kuhakikisha wanasimamia malengo ya ukusanyaji wa mapato yaliyowekwa kwenye Mamlaka za Serikali za Mitaa.
Bashungwa ameyasema hayo leo tarehe 4 Julai, 2022 alipokuwa akizungumza na Sekretarieti ya Mkoa wa Iringa kabla ya kuanza ziara ya kikazi katika Halmashauri ya Wilaya ya Iringa kwa lengo la kukagua miradi ya maendeleo inayotekelezwa katika jalmashauri hiyo.

Amesema kuwa mwaka mpya wa fedha unaanza hivyo ni vyema Wakuu wa Mikoa na Wakuu wa Wilaya wakajipanga kuhakikisha wanazisimamia Halmashuri zao ili ziweze kutekeleza malengo yaliyowekwa na Serikali.

"Mwaka mpya wa fedha umeanza ni wajibu wa Wakuu wa Mikoa na Wakuu wa Wilaya zote nchini kuhakikisha wanazisimamia kikamilifu Halmshauri zao katika ukusanyaji wa mapato ili kufikia malengo yaliyowekwa na Serikali." amesema Waziri Bashungwa.

Vilevile, Waziri Bashungwa amewaagiza viongozi hao kuhakikisha wanasimamia miradi ya maendeleo inayotekelezwa na Halmashauri ili ilete tija kwa wananchi.

Amewataka viongozi hao kuhakikisha wanawashirikisha Mameya na Wenyeviti wa Halmashauri wakati wa ziara za viongozi wa Kitaifa kwa kuwa ndio wawakilishi wa wananchi, hivyo amewataka itifaki ifuatwe.

Aidha, amewataka kuhakikisha fedha za makusanyo ya ndani zinaelekezwa kwenye miradi ya maendeleo kama miongozo inavyoelekeza.
Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia langolahabari@gmail.com au WhatsaApp: +255 621 896 990

Pages