Breaking

Thursday, 14 July 2022

SHAMBA LA MITI LA HEKA 10 LATEKETEA KWA MOTO KAGERA, MWEKEZAJI ATOA OMBI KWA SERIKALI


Na Lydia Lugakila, Lango la habari

Uchomaji moto wa misitu ya hifadhi na maeneo yaliyohifadhiwa kisheria umekuwa ukileta athari za kimazingira katika maeneo mbali mbali hapa nchini.

Kila mwaka majira ya kiangazi kuna matukio ya uchomaji moto ovyo misitu na mapori yanasababisha hasara kubwa.

Pamoja na jitihada kubwa zinazofanywa na serikali kupitia wakala wa huduma za misitu Tanzania TFS bado kuna kiwango kikubwa cha uharibifu wa mazingira bado kuna tatizo la ukataji miti ovyo na uchomaji moto misitu hasa ya asili.

Sekta ya misitu inachangia asilimia 3.5 ya pato la taifa, hivyo ni dhahiri kuwa sekta hiyo ni fursa mojawapo ambayo ikitumika kikamilifu itachangia zaidi katika kukuza uchumi.

Katika maeneo tofauti tofauti hapa nchini yamekuwa yakijitokeza matukio ya uchomaji moto yanayosababisha kuwakatisha tamaa wawekezaji.

Hali hii inamkuta mwekezaji na mmiliki wa shamba la miti mchungaji Dionizi Karwani ambaye pia ni mkurugenzi wa shule ya sekondari St. Cecilia aliyewekeza katika kata ya Buhendangabo tarafa ya Bugabo halmashauri ya wilaya ya Bukoba Mkoani Kagera baada ya kupata hasara ya milioni 20 iliyotokana na kuteketea kwa shamba la miti aina ya mipain lenye heka 10.


Mchungaji Karwani anasema aliamua kuwekeza miti hiyo tangu mwaka 2019 lengo likiwa ni kutunza mazingira na kuongeza kipato na kuwezesha upatikanaji wa ajira.

Anasema kuwa ndoto yake inakwenda vibaya baada ya moto uliozuka julai 9, 2022 kumuingiza katika hasara.


Kilio chake kikubwa kwa serikali juu ya watu wanaojihusisha na wachomaji Moto misitu na mapori ni kuomba kutungiwa sheria inayowabana wanaoharibu mazingira kwani wawekezaji wanajitahidi kuwekeza na kutekeleza sera ya kutunza mazingira japo wanakutana na vikwazo.

"Viongozi waweke umakini kwa wanaochoma moto ili hatua kali zichukuliwe dhidi yao" alisema mchungaji Karwani.

Pia anawaomba wananchi wasifumbie macho vitendo ya uchomaji moto ili atakayebainika achukuliwe hatua kali za kisheria.


Deusdedith Rwazi ni mwananchi na mkazi wa Kijiji Rushaka kata Buhendangabo tarafa ya Bugabo anasema tukio la moto linaathiri mazingira na kuleta hasara katika jamii huku akilalamikia ushirikiano haba wa wananchi unapotokea moto wamekuwa hawatoi ushirikiano mzuri huku wengine wakibaki kusema mwenye miti azime mwenyewe.

Theophil Elieza ni diwani wa kata ya Buhendangabo tarafa ya Bugabo halmshauri ya wilaya ya Bukoba anasema ushirikiano wa haraka unahitajika Kati ya viongozi wa kata na vijiji huku mikutano ikiendelea kufanyika ili kuwataka wanaochoma moto kuacha mara moja.

"Tunatakiwa tukutane na wenyeviti wa vijiji na watendaji katika kata ya Buhendangabo, Kaagya na Nyakato ili tuone namna ya kutatua tatizo la moto" alisema diwani Elieza.

Kwa upande wake mhifadhi mkuu shamba la miti Rubare Bi Mandaro Salum ametoa pole kwa mwekezaji huyo na wengine waliopata hasara ya mioto na kuwa tayari jeshi la zimamoto mkoa wa Kagera wanaandaa mpango wa kutoa elimu kupitia vyombo vya habari ili wananchi waelewe madhara yatokanayo na uchomaji moto.

Bi Mandaro anasema wananchi walio wengi wamekuwa hawajua wakati mzuri wa kuandaa shamba na wengine kutoona umuhimu wa kupata huduma kwa wataalam wa misitu na kuwa atakayebainika anaandaa shamba bila taarifa kifungo ni miaka 15 jela.

Ameongeza kuwa elimu kwa wananchi bado ni ndogo kwani baadhi ya wananchi wakielezwa juu ya utoaji taarifa kabla ya kuandaa shamba ambapo baadhi hubaki kusema "shamba la kwangu mwenyewe na nikianza kuandaa nitoe taarifa?

Anasema serikali inatakiwa kushirikiana na taasisi zisizo za kiserikali na kuomba sheria ndogo za halmshauri ziwatake wananchi wasiandae shamba bila kuomba kibali kwa mtendaji ili kama moto utamuelemea mtu apate msaada kutoka kwa jamii.

Hata hivyo naye mhifadhi wa misitu shamba la miti Rubare Hamidu Miraji Shaluwa anawashauri wananchi kuchukua tafadhali katika kipindi hiki cha kiangazi kwani ni hatari katika uchomaji mioto na kushauri wananchi kutoanzisha moto ambao hawataweza kuumudu.
Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia langolahabari@gmail.com au WhatsaApp: +255 621 896 990

Pages