Breaking

Monday, 25 July 2022

SERIKALI YATOA TAMKO TISHIO LA MGOMO WA MADEREVA, WACHOCHEZI KUKIONA



Serikali imetoa tamko juu ya tishio la mgomo wa madereva, ambao umetajwa kupokewa tofauti na baadhi yao ukilenga katika viwango vya posho ambavyo Madereva, Wamiliki wa Vyombo vya Usafiri na Serikeli waliafikiana katika vikao vya majadiliano.

Taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya Habari na Waziri wa Nchi, ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na wenye ulemavu Prof. Joyce Lazaro Ndalichako, imesisitiza kuwa nafasi ya majadiliano bado ipo wazi na hivyo Wafanyakazi Madereva ambao wana hoja na malalamiko zaidi ya yale yaliyofanyiwa kazi, wayawasilishe rasmi katika mamlaka zinazohusika ili yaweze kupatiwa ufumbuzi.

TAZAMA VIDEO

Aidha Ndalichako, amewasihi madereva kupokea kwa mtazamo chanya taarifa ya Serikali kuhusu hatua zilizochukuliwa katika kushughulikia Hoja na Malalamiko yaliyowasilishwa na Vyama vyao, na Wamiliki wa Vyombo vya Usafirishaji huku akiwataka kuendelea kutekeleza majukumu yao kama kawaida.

Ametoa rai kwa makundi yanayojihusisha kuchochea migomo ya Madereva kuacha mara moja kwani kufanya hivyo ni kukiuka Sheria na kuongeza kukwa Serikali haitasita kuchukua hatua stahiki kwa wale wote watakaoendelea kuchochea migomo ya Madereva.

Ikumbukwe kuwa tarehe 22 Julai, 2022 Serikali ilitoa taarifa kwa Vyombo vya Habari kuhusu hatua zilizochukuliwa katika kushughulikia Hoja, na Malalamiko yaliyowasilishwa na Viongozi wa Vyama vya Wafanyakazi Madereva na Wamiliki wa Vyombo vya Usafirishaji nchini, ambapo walikubaliana waajiri hawaruhusiwi kulipa viwango vya chini vya posho za safari.
Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia langolahabari@gmail.com au WhatsaApp: +255 621 896 990

Pages