Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Mhandisi Robert Gabriel amemtaka Mkandarasi CCECC kuongeza spidi ya Ujenzi wa Daraja la JPM lenye urefu wa KM 3.2 na wafanyakazi kuwa wazalendo katika kuhakikisha vifaa vya ujenzi kwenye mradi huo vinatunzwa.
Ametoa wito huo Julai 4, 2022 wakati wa ziara yake aliyoambatana na Kamati za Usalama za Mkoa na wilaya za Sengerema na Misungwi kwenye daraja hilo iliyolenga kuona namna kazi inavyofanywa katika kuwaunganisha wananchi wa Kigongo na Busisi.
"Niendelee kulipongeza jeshi la Polisi na kuanzia leo tutaongeza ulinzi kwenye daraja hili ili kuhakikisha wakati vyuma na vifaa vingi zaidi vinatumika panabaki kuwa salama na eneo la mita 300 kulia na kushoto mwa daraja hili litakua kwenye ulinzi ikiwa ni kwa usalama wa wavuvi pia." Amesisitiza Rc Gabriel
Amesema kuwa mtu yeyote atakayekamatwa na kifaa ambacho asili yake ni kwenye mradi huo atachukuliwa hatua za kisheria hivyo amewataka wafanyakazi darajani hapo kuridhika na mishahara na kuwa wazalendo kwa kulinda vifaa.
"Uzalendo hapa uwe ndio dira yetu, viongozi na wananchi tuwe wasimamizi wa pamoja kwenye mradi huu ili kuhakikisha vifaa na mitambo vinatunzwa na mradi unakamilika ndani ya muda uliokusudiwa." Mhe Robert.
Awali, Mkandarasi Mshauri wa Mradi Abdulkarim Majuto amefafanua kuwa ujenzi wa daraja la JPM umefikia asilimia 47.4 na kwamba nguzo 21 kati ya 67 tayari zimewekwa na ndani ya mwezi Julai zitawekwa nguzo ulalo na zege ya juu.
Source: Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Mwanza