Na lango la habari
Katika hafla ya kukabidhi boti kwa ajili ya doria za kudhibiti uvuvi haramu, iliyotolewa na Serikali kupitia Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Mkuu wa Mkoa wa Kagera Meja Jenerali Charles Mbuge amewahimiza wananchi kuendelea kuunga mkono juhudi za Serikali kupiga vita uvuvi haramu katika ziwa Victoria.
Akizungumza katika hafla hiyo iliyofanyikia katika soko la Magalini lililopo kijiji Katembe, Kata ya Nyakabango, amewahimiza wananchi kuhakikisha kila mmoja anakuwa mlinzi wa mwenzake wa maliasili zilizomo ziwani ili kuweza kuzuia vitendo vya uvuvi haramu unaofafanyika katika ziwa Victoria.
"Naomba mkawambie na wananchi ambao hawakufika hapa wawe wazalendo kwa maliasili zetu tukijiingiza katika vitendo vya uvuvi haramu hatutapata samaki kwa miaka ijayo wala watoto wetu hawataona samaki hao na pia hatutakuwa na lishe bora kwenye miili yetu samaki ni lishe kwa afya zetu" ameeleza Meja Jenerali Mbuge
Aidha, amesema kuwa wale wote watakaokamatwa wakishiriki kufanya uvuvi haramu sheria itachukua mkondo wake na kuelekeza mamlaka zisiwasamehe, taratibu zote zifuatwe bila kumuonea aibu mvuvi haramu yeyote.
Sambamba na hayo ameishukuru Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inayoongozwa na Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan kupitia wizara ya Mifugo na Uvuvi kwa kutambua umuhimu wa kuwa na boti ya kufanya doria kudhibiti uvuvi haramu ili hata vizazi vijavyo viweze kunufaika na mazao ya samaki.
Taarifa iliyosomwa na Masanja Lukasi Kadashi Afisa Mfawidhi wa Uvuvi, Wizara ya Mifugo na Uvuvi imeeleza kuwa wamefanikiwa kupata boti yenye injini ya (Hos Power 40) kutoka kwa ajili ya kuendeshea doria za udhibiti wa uvuvi haramu yenye uwezo wa kubeba watu 6 na boti hiyo imegarimu kiasi cha Tsh. Milioni 32.9
Pa amesema kuwa kabla ya kupata boti hiyo uvuvi haramu ulikuwa unafanyika hadharani hali iliyopelekea kushindwa kuwakamata watuhumiwa kwa urahisi na wakati mwingine watuhumiwa kukimbia lakini baada ya kupata boti hiyo itasaidia sehemu kubwa kukomesha uvuvi haramu na pia itasaidia kuwakamata hata wanaotorosha na kusafirisha samaki kimagendo.
Kwa upande wake Mkuu wa wilaya ya Muleba Mhe. Toba Nguvila ameeleza kuwa Halmashauri tayari imetoa kiasi cha Tsh. Milioni 40 kwa ajili ya kujenga eneo la kuchambulia dagaa na tayari upo mpango wa kuboresha barabara ya kuingia katika soko hilo kwa kiwango cha changarawe.
Naye Afisa Uvuvi wa Wilaya Ndg. Wilfred Tibendelana katika taarifa ameeleza kuwa Halmashauri imeweza kufanya doria 145 na kufanikiwa kukamata zana haramu Kokoro 214, timba 842, nyavu ndogo za makila 655, na nyavu ndogo za dagaa 21 na mitumbwi 92 katuli20 Tupatupa 18 na samaki kilo 5783. Nyavu haramu zilizokamatwa zinakadiliwa kuwa na thamani ya Tsh. Bilioni 2,126,007,500.
Pia ameongeza kwa kusema kuwa kwa mwaka wa fedha 2021/2022 tangu soko la Magarini kurejeshwa kuendelea na shughuli za uzalishaji Halmashauri imeweza kukusanya mapato ya tozo ya ushuru wa samaki dagaa na mazao mengine kiasi cha Tsh. Milioni 113.5na kabla ya soko kufunguliwa Halmashauri ilikuwa,ikikusanya kiasi cha Tsh. 68.5 kwa mwaka.