Breaking

Thursday, 14 July 2022

POLISI WAUA JAMBAZI ALIEVAMIA DUKA NA KUIBA MILLIONI 19 KAGERA, WATATU WAFANIKIWA KUKIMBIA



Na Samir Salum, Lango la habari

Mtu mmoja anayedhaniwa kuwa ni jambazi ambaye majina yake hayajafahamika ameuawa kwa risasi na polisi Mkoani Kagera baada ya yeye na wenzake watatu kuvamia duka Wilayani Biharamulo na kuiba Tsh. milioni 19 na vocha za simu.

Akithibitisha hilo Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kagera ACP William Mwampaghale amesema kuwa tukio hilo limetokea Mnamo Julai 12,2022 majira ya saa 01:45  ambapo watu wanne wanaosadikika kuwa majambazi walivamia na kuvunja duka la Mfanyabiashara Musa Maduhu katika kijiji cha Nemba Wilaya ya Biharamulo.

Kamanda amesema Watu hao walipofika kwenye duka la mfanyabiashara huyo walilipua baruti na kumfanya mlinzi kukimbia akihofia usalama wake ndipo walivunja duka hilo na kupora kiasi cha fedha shilingi 19,377,250/= pamoja na vocha za mitandao ya simu ya Airtel na Tigo ambazo bado hazijafahamika thamani yake.

"Jeshi la Polisi baada ya kupokea taarifa za tukio hilo liliweka mtego na ndipo majira ya saa 04:00 huko katika kijiji cha Mgera, Kata ya Nyantakara lilifanikiwa kuwaona watuhumiwa hao wakiwa wanakimbia wakiwa kwenye pikipiki moja yenye namba za usajili MC.489 DJH aina ya Kinglion"amesema

Kamanda Mwampaghale amesema watuhumiwa hao walisimamishwa lakini walikataa kusimama ndipo askari walipiga risasi juu mara tatu lakini watu hao waliendelea kukaidi huku wakilipua baruti hali iliyopelekea Askari walifyatua risasi na kuwajeruhi watu wawili.

"Mtu mmoja ambae hajafahamika jina anayekadiriwa kuwa na umri kati ya miaka 30 – 35 alifariki dunia wakati anapelekwa hospitali huku mwingine mmoja akiwa amejeruhiwa kwa risasi alikimbilia msituni Watuhumiwa wengine wawili walifanikiwa kutoroka na wanaendelea kutafutwa" ameelezea Kamanda Mwampaghale

Katika eneo la tukio kulipatikana pikipiki iliyotumiwa na wahalifu hao yenye namba za usajili MC.489 DJH ,fedha noti mbalimbali za TSH.355,000/= na sarafu TSH.22,250/= jumla TSH.377,500/= ambazo zilikuwa kwenye mfuko wa pinki, vocha 30 za mtandao wa Tigo za shilingi 500/= kila moja,simu mbili, shoka moja,sururu moja na mtambo wa kulipulia baruti.

Kamanda amesema kuwa Jeshi la Polisi Mkoa wa Kagera linaendelea na msako mkali wa kuwatafuta watuhumiwa hao waliotoroka ili sheria ichukue mkondo wake.

Aidha ametoa onyo kwa watu wote wanaojihusisha na ujambazi kuacha mara moja na kutafuta njia halali za kujipatia kipato huku akiwaomba wananchi kuendelea kutoa taarifa za uhalifu na wahalifu kwenye maeneo yao ili hatua kali za kisheria zichukuliwe dhidi yao.
Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia langolahabari@gmail.com au WhatsaApp: +255 621 896 990

Pages