Katibu Mkuu Wizara ya Madini Adolf Ndunguru amezipongoza Taasisi zilizopo chini ya Wizara ya Madini kwa ushirikiano waliouonesha katika Mwaka wa Fedha uliopita (2021/22) kwa kufanikisha kufikia malengo ya makusanyo.
Ndunguru ametoa pongezi hizo leo Julai 23, 2022 wakati akifungua kikao cha Wataalamu wa Sekta ya Madini wa Wizara hiyo na Taasisi zilizo chini yake kilichofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Wizara Mtumba jijini Dodoma.
Ndunguru amewataka wataalamu wa Sekta ya Madini kuendeleza ushirikiano katika utendaji kazi wao ili mwisho wa siku waweze kufikia malengo waliyopangiwa na serikali.
Kwa upande wake, Kamishna wa Madini Dkt. Abdulrahman Mwanga amesema kikao hicho kimelenga kujadili mikakati ya kufanya ili kufanikisha kukusanya maduhuli ambayo kwa Mwaka wa Fedha (2022/23) wizara imepangiwa kukusanya kiasi cha Tsh milioni 822,018,203,000.
Aidha, Dkt. Mwanga amesema kikao hicho kitajenga umoja wa pamoja na kuweka mikakati ya kuwezesha upatikanaji wa ongezeko la makusanyo ya mapato yatokanayo na Sekta ya Madini ambapo Mwaka wa Fedha 2021/22 wizara ilipangiwa kukusanya kiasi cha Tsh 650,010,002,000.
Pia Dkt. Mwanga amewataka wataalamu wa Sekta ya Madini kuwa huru kujadili mafanikio na changamoto zinazowakabili na kuzitafutia ufumbuzi ili sekta hiyo iweze kusonga mbele kwa mafanikio na hatimaye iweze kufikia makadirio ya makusanyo iliyopangiwa na Serikali.
Naye, Katibu Mtendaji wa Tume ya Madini Mhandisi Yahya Samamba amesema Tume ya Madini imeweka mikakati ya kuimarisha usimamizi wa mnyororo wa shughuli za madini ambapo itashirikisha Vyombo vya Ulinzi na Usalama na Halmashauri za maeneo husika ili kudhibiti upotevu wa fedha za serikali zitokanazo na Sekta ya Madini nchini.
Kikao hicho, kimehudhuriwa na wataalamu kutoka Wizara ya Madini, Tume ya Madini, Shirika la Madini la Taifa (STAMICO), Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa Madini Tanzania (GST)