Naibu Waziri wa ujenzi na uchukuzi Mhandisi Godfrey Kasekenya amewaagiza wakala wa barabara nchini Tanroad pamoja na wakala wa barabara mjini na vijijini Tarura kuhakikisha wanafanyia kazi taarifa zinazotolewa na wananchi kuhusu marekebisho ya barabara haraka baada ya kupokea taarifa za ubovu wa barabara kupitia mfumo mpya wa kielektoniki.
Naibu Waziri Kasekenya ametoka kauli hiyo jijini Mwanza wakati wa warsha ya kujadili namna ya kukabiliana na madhara ya mabadiliko ya tabianchi kwenye miundombinu ya barabara pamoja na uzinduzi wa mfumo wa kielektroniki wa ufatiliaji wa hali ya barabara nchini.
Kwa upande wake mwenyekiti wa bodi ya barabara nchini Joseph Haule amesema sekta ya barabara ni nyenzo muhimu kwa maendeleo ya kijamii na kiuchumi.
"Bila usafiri wa uhakika wa barabara, ni vigumu wananchi kunufaika na huduma za kijamii na kiuchumi ambazo zinatolewa na kuwezeshwa na Serikali ikiwemo elimu, afya na upatikanaji wa masoko,"amesema Haule.
Haule amesema miundombinu hiyo inakabiliwa na changamoto zinazopelekewa na mabadiliko ya tabia ya nchi katika nchi mbalimbali duniani kama mvua kubwa,joto kali,upepo mkali pamoja na kuzidishwa kwa uzito wa magari barabarani.
Takwimu zilizotilewa katika warsha hiyo zinaonesha kuwa mwaka kwa 2020 thamani ya mtandao wa barabara zilizorasimishwa ni trilioni 21 sawa na asilimia 16.
Mkutano huo umewakutanisha wadau wa barabara nchini kutoka TANROAD pamoja na TARURA kote nchini.