Na Catherine Sungura,Siha
Madaktari na watoa huduma wote nchini wametakiwa kuendelea kuwa wenye upendo, kujituma, kujitoa na kuzingatia weledi na maadili ya tasnia ya utabibu.
Kauli hiyo imetolewa na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe.Dkt. Philip Isdor Mpango mwishoni mwa mwiki wilayani Siha wakati akiongea na watoa huduma wa afya pamoja na wananchi wa Wilaya hiyo.
Dkt. Mpango alisema kuwa anafahamu wako madaktari na wahudumu wa afya wengi wanaofanya kazi nzuri na wengine hata katika mazingira magumu na hatarishi.
"Mnafanya kazi ya Mungu na endeleeni kufanya hivyo bila kukata tamaa. Pamoja na Serikali kuendelea kuboresha maslahi yenu, nawasihi pia motisha yenu iwe katika kuona thamani ya maisha ya watu wengi mliyookoa kwa huduma za afya mnazotoa".
Aidha, aliwataka madaktari na wahudumu wote kutumia utaalamu wao kutoa elimu ya afya na kinga.
Alisema ni wazi kuwa, gharama za tiba kwa mtu aliyepata maambukizi ya ugonjwa ni kubwa na wakati mwingine hazibebeki kwa watanzania walio wengi hivyo Wizara ya Afya, madaktari na wahudumu wa afya waongeze jitihada za kutoa elimu ya afya hususan ile inayolenga katika kuwakinga watanzania na magonjwa ya kuambukiza na hata yasiyoambukiza ili kuepuka gharama kubwa za matibabu.
"Kuweni wabunifu katika kutoa elimu, tumieni njia mbalimbali ikiwemo mitandao ya kijamii, teknolojia ya Habari na mawasiliano pamoja na mifumo ya kidigitali"Tukumbuke ule msemo wa wahenga wetu kuwa, “Kinga ni bora kuliko tiba”.