Breaking

Saturday, 23 July 2022

MAKAMU WA RAIS AKEMEA UVAMIZI WA MAENEO YA HIFADHI..AAGIZA KUTOLEWA ELIMU YA BIASHARA YA HEWA UKAA



Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Philip Mpango amemuagiza waziri mwenye dhamana ya mazingira Selemani Jafo kwa kushirikiana na watumishi wote wa wizara hiyo kuhakikisha wanatoa elimu kwa wananchi nchi nzima waweze kufahamu fursa zilizopo katika biashara ya hewa ukaa.

Dkt. Mpango amesema hayo wakati akikabidhi mfano wa hundi ya jumla ya shilingi bilioni 2.3 kwa halmashauri ya wilaya ya Tanganyika pamoja na vijiji nane vya wilaya hiyo fedha zilizotokana na biashara ya hewa ukaa.

Ameitaka wizara kuhakikisha mapungufu ya kisera na usimamizi wa biashara ya hewa ukaa yanapatiwa ufumbuzi ili taifa liweze kunufaika na biashara hiyo.

Ametoa wito kwa halmshauri zingine hapa nchini kujifunza kutoka Halmashauri ya Tanganyika mkoani Katavi namna ya kufaidika na biashara hiyo.

Aidha ametoa wito kwa wizara ya maliasili na utalii kwa kushirikiana na serikali za mikoa kuwachukulia hatua kali za kisheria waharibifu wa mazingira ikiwemo wanaochoma moto misitu pamoja na kusimamia sera na sheria ya mazingira ili kupunguza na kuondoa athari za kimazingira zinazoweza kujitokeza.

Pia Makamu wa Rais ameagiza mkoa wa Katavi kufanya tathimini ya kimazingira na kutoa elimu ya utunzaji wa mazingira kwa kushirikisha moja kwa moja jamii.

Katika hatua nyingine Makamu wa Rais Dkt. Mpango amekemea vitendo vya wananchi kuvamia maeneo ya hifadhi kwaajili ya shughuli za ufugaji na kilimo.

Makamu wa Rais amewataka baadhi ya viongozi wa serikali na chama wanaruhusu wananchi kuvamia maeneo ya hifadhi kuacha vitendo hivyo mara moja kwani vinahatarisha amani pamoja na kuchochea uharibifu wa mazingira.

Akitoa taarifa ya mradi wa hewa ukaa katika Halmashauri ya Wilaya ya Tanganyika, Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo Shaban Juma amesema malengo ya mradi huo ni pamoja na kuhifadhi na kulinda misitu, bioanuai zote zilizo hatarini kutoweka wakiwemo sokwe mtu, kutunza vyanzo vya maji, kushirikisha jamii katika katika uhifadhi na kunufaika moja kwa moja na faida za uhifadhi.

Ameongeza kwamba mradi unaiwezesha jamii kufanya shughuli za maendeleo ya vijiji kupitia mapato yatokanayo na uuzwaji wa hewa ukaa.

Mkurugenzi huyo amesema kupitia mradi huo halmshauri imekusanya zaidi ya milioni mia tatu tisini na nane ambazo zimesaidia katika uendeshaji wa halmashauri, utoaji wa bima za afya kwa wakazi wote waishio katika vijiji nane vya mradi huo, kujenga madarasa, kituo cha afya kata ya katuma pamoja na zahanati nne katika vijiji ili kusogeza huduma za afya karibu na wananchi.

Biashara ya hewa ukaa katika Halmashauri ya Wilaya ya Tanganyika ilianza mwaka 2018 ikiendeshwa na halamshauri hiyo na taasisi ya Carbon Tanzania kwa kushirikiana na mradi wa Tuungane kwa Afya na Mazingira bora.

Jumla ya hekta 216,944 za misitu zimehifadhiwa katika vijiji nane vya tarafa ya Mwese na wananchi 34,242 wananufaika na biashara hiyo.

Awali Makamu wa Rais Mhe. Dkt. Philip Mpango alisimama kuwasalimu wananchi wa Kijiji cha Ifukutwa kilichopo Wilaya ya Tanganyika mkoani Katavi ambao walijitokeza barabarani kumlaki akiingiia katika Wilaya hiyo.

Akiwa kijijini hapo, Makamu wa Rais ameiagiza Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi kuharakisha ujenzi wa barabara ya kutoka Katavi kuelekea Uvinza Kigoma ili kuwasaidia wananchi shughuli za usafirishaji wa mazao pamoja na kufanya biashara kwa urahisi.

Aidha Makamu wa Rais amesisitiza suala la elimu kwa watoto wa Wilaya hiyo kwa kuwaasa wazazi na walezi kuhakikisha wanafuatlia maendeleo ya Watoto wao katika elimu pamoja na kusimamia wahitimu vema.

Amesema mkoa huo unakabiliwa na changamoto ya Watoto wa kike kushindwa kumaliza masomo kutokana na sababu mbalimbali kama ikiwemo ujauzito hivyo hakuna budi kupiga vita vitendo hivyo kwa nguvu zote.

Pia Makamu wa Rais amewasihi kuzingatia lishe ili uzalishaji mkubwa wa chakula wanaoufanya uendane na afya zao.
Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia langolahabari@gmail.com au WhatsaApp: +255 621 896 990

Pages