Breaking

Saturday, 9 July 2022

BALOZI MULAMULA AKOSHWA NA MAONESHO YA KIBIASHARA KAGERA AHAIDI KUSHUGHULIKIA VIKWAZO IKIWEMO VIZUIZI

Na Lydia Lugakila, Lango la habari


Waziri wa mambo ya nje na ushirikiano wa Afrika Mashariki (Mb) balozi Liberata Mulamula Rutageruka ametoa kauli hiyo akiwa Mgeni rasmi katika hitimisho la maonesho ya kwanza ya kibiashara ya jumuiya ya Afrika mashariki yaliyomalizika julai 8, 2022.


Balozi Mulamula akitoa hotuba yake katika maonyesho hayo ametaja kuvutiwa zaidi na bidhaa za asili kutoka kwa akina mama wajasiriamali ambao wamejiongeza katika kuongeza thamani bidhaa, kuahidi kushughulikia changamoto mbali mbali ambazo ni kikwazo katika biashara ikiwemo wingi wa vizuizi mipakani.


" Nawapongeza sana waandaaji pia washiriki naahidi kushughulikia na changamoto za kibiashara  zilizobainika na nitaanza na upatikanaji wa alama ya TBS na kuhusu vizuizi ni kweli vipo hapa nchini na vinawatajirisha wanaosimama katika vizuizi hivyo.


Amesema kuwa kwa bidhaa alizozishuhudia katika maonyesho hayo ni lazima zivuke mipaka kwani hadi Sasa nchi ya Ghana ina uhaba mkubwa wa mazao ya chakula na kuwa mkoa wa Kagera una fursa nyingi hivyo ni vyema wananchi Mkoani humo na watanzania kwa ujumla kuwekeza zaidi kwa kuongeza uzalishaji katika viwango vinavyokidhi soko la kimataifa.


Ameongeza kuwa kwa hatua iliyofikiwa kutokana na ushiriki wa nchi za jumuiya ya Afrika Mashariki katika biashara ni fursa kwani wameonyesha kwamba Diplomasia ya uchumi inazidi kukua na kuimalika.


Akiwasilisha risala mbele ya Mgeni rasmi mratibu wa maonyesho hayo William Oswald Rutta amesema hadi kufungwa kwa maonyesho hayo wamefanikiwa kupata watu zaidi ya 7,000 ambapo malengo yao yalikuwa ni mzunguko wa fedha mafanikio katika kukuza uchumi wa Mkoa wa Kagera, kuhamasisha wawekezaji kujenga hoteli kubwa ili kuwavutia watalii wa nje na ndani.


Rutta ameiomba serikali kuondoa na kupunguza vizuizi kwani vimewafanya vijana wengi kuondokana na shughuli za barabarani huku akiahidi kuwa maonyesho yajayo yatawawezesha wananchi kutembelea hifadhi za taifa.


"Nikuombe Mh, utusaidie kutengeneza Route ya ndege ya kutoka Kilimanjaro kuja Kagera walau mara tatu kwa wiki ili kuongeza watu kuja kutalii pamoja na kuwepo mabasi yatokayo Bukoba kwenda Kampala kama ilivyokuwa kipindi cha nyuma.


Naye  mkuu wa Mkoa wa Kagera Meja Jenerali Charles Mbuge amepongeza ubunifu wa waandaaji na kuwa maonyesho hayo yameongeza wigo mpana kwa wafanya biashara na kuahidi kufanya vizuri zaidi mwaka hujao.


Hata hivyo maonyesho hayo yalianza juni 15  na kufungwa Julai 8, 2022.

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia langolahabari@gmail.com au WhatsaApp: +255 621 896 990

Pages