Na Mwandishi wetu, Dar es Salaam
Baada ya Kamati ya utatu kufanya majadiliano baina ya viongozi wa vyama vya wafanyakazi, madereva na wamiliki wa vyombo vya usafirishaji, Serikali imeamuru wamiliki wa magari kuwalipa madereva wa magari yanayotoka Tanziania kuelekea nchini Kongo, sh 700,000 (Millage) na posho ya overstay baada ya siku 20 Dolla 10 za kimarekani kwa siku ambapo posho za return na kupakia na kushusha mzigo hazijafikiwa muafaka.
Kauli hiyo imetolewa na Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi Vijana Ajira na watu wenye ulemavu Potras Katambi wakati akieleza hatua zilizochukuliwa na Serikali kuhusu hoja na malalamiko yaliyowasilishwa na wafanyakazi madereva na wamiliki wa vyombo vya usafirishaji nchini.
Amesema kuwa, hatua hiyo imekuja mara baada ya Serikali kusimamia kamati ya utatu ilioundwa kusimamia posho za safari kwa madereva baina ya viongozi wa vyama vya wafanyakazi, madereva na wamiliki wa vyombo vya usafirishaji nchini.
"Kuhusu posho za returns madereva walihitaji sh 350,000 na upande wa waajiri walifikia sh 300,000, na posho ya kushusha na kupakia mzigo madereva walihitaji dola 200 za kimarekani na waajiri walifikia dola 150 za kimarekani mpaka sasa hakuna muafaka uliofikiwa katika hili"amesema Naibu Waziri Katambi.
Ameongeza kuwa, viwango hivyo vya posho ni sehemu ya hali bora kwa wafanyakazi madereva ambavyo vitapaswa kuzingatia na waajiri katika mikataba ya ajira za madereva, ambapo Serikali itaendelea kufanya ukaguzi wa kazi ikiwa ni pamoja a kukagua mikataba hiyo kama imezingatia makubaliano hayo.