Polisi katika kaunti ya Kirinyaga wamemkamata mwanamume mmoja mwenye umri wa miaka 45 kwa kuhifadhi mwili wa mamake na kusali kuwa afufuke.
James Muchira na mkewe walikamatwa katika kijiji cha Mutithi usiku wa Jumatatu, Julai 4, 2022 baada ya jamaa zao wakiongozwa na nduguye Evans Mwaniki kumwomba naibu chifu wa eneo hilo kuingilia kati.
Kwa mujibu wa ripoti, mshukiwa alikataa kumruhusu yeyote katika makaazi yake ambayo pia huhudumu kama kanisa kwa jina "God's mountain of Believers."
“Maafisa wangu walishtuka kupata mwili uliooza,” kamanda wa polisi wa kaunti ndogo Mwea Magharibi Wilson Koskei.
Mshukiwa anaripotiwa kumtoa mamake hospitalini ambako alikuwa akipokea matibabu ili amwombee katika kanisa lake la nyumbani.
“Siamini katika kanisa lake la familia,” Mwaniki alisema.
Wanakijiji waliopigwa na butwaa walishangaa ni vipi familia hiyo ilifanikiwa kuishi na mwili huo licha ya uvundo uliokuwa nyumbani kwao.
Ili kuwalinda kutoka kwa wakaazi waliokuwa na ghadhabu tayari kuwaangamia, Muchira, mkewe na mwanake mwengine walipelekewa kwa haraka katika kituo cha Kiamaciri.
“Acha tuchunguze ili tujue mashtaka ya kuwafikisha nayo mahakamani au watashtakiwa kwa makosa ya kutesa maiti,” Koskei alisema.
Mwili wa Tabitha Wakathare ulipelekwa katika makafani ya Hospitali ya Kerugoya unakosubiri kufanyiwa uchunguzi.