Watu 14 wamekufa kwenye ajali ya helikopta ya jeshi iliyotokea nchini Mexico saa chache baada ya kukamatwa kwa kiongozi wa genge la biashara ya dawa za kulevya aliyekuwa akisakwa kwa muda mrefu.
Taarifa iliyotolewa na jeshi la Mexico imesema wote waliokufa kwenye ajali hiyo walishiriki operesheni ya kukamatwa kwa Caro Quintero ambaye ni mwanzilishi mwenza wa genge kubwa la ulanguzi wa dawa za kulevya.
Katika ajali hiyo iliyotokea kwenye jimbo la kaskazini magharibi mwa Mexico la Sinaloa mtu mmoja amenusurika lakini inaarifiwa amepata majeraha makubwa na tayari ameanzishiwa matibabu.
Rais wa Mexico Andrés Manuel López ametuma salamu za rambirambi kwa familia za wote waliokufa na taarifa zinasema uchunguzi umeanzishwa kubaini chanzo cha mkasa huo.