WAZIRI wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhandisi Hamad Masauni ameitaka Idara ya Uhamiaji nchini kusimamia uingiaji na utokaji wa wageni katika mipaka ya nchi kwa kufuata sheria za nchi.
Waziri Masauni ameyasema hayo leo Jumatano Juni 15, 2022 Loliondo, Ngorongoro mkoani Arusha alipofika kukagua maendeleo ya Zoezi la Uwekaji wa Alama za Mipaka katika eneo la Pori Tengefu la Loliondo.
Waziri Masauni ameeleza kuridhishwa kwake na maendeleo ya zoezi na kuwataka wahusika kuhakikisha kuwa zoezi hilo linakamilika kwa wakati.
Aidha, amesema kuwa serikali itafanya uhakiki wa kina kubaini uendeshaji wa Asasi za Kiraia nchini kufanya kazi zao kwa mujibu wa sheria na zile zitakazokiuka zitachukuliwa hatua kali za kisheria.
Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Ngorongoro Mwalimu Raymond Mangwala aliyemwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Arusha John Mongela, alimueleza Waziri Masauni kuwa amepokea maelekezo yake na kwamba atahakikisha kuwa hali ya usalama wa wananchi na mali zao inaendelea kuimarishwa wilayani Ngorongoro na kuwa zoezi hilo litaendelea kwa hali ya amani na utulivu.