WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Mhe. Innocent Bashungwa amemuagiza Katibu Tawala wa Mkoa Kagera, Prof. Faustine Kamuzora kuwasimamisha kazi Afisa Manunuzi wa Halmashauri ya Wilaya Karagwe, Bi.Magreth Bukuku na Mkaguzi wa ndani wa Halmashauri ya Wilaya Karagwe, Bw. Dickson Sabe kuanzia leo Juni 11, 2022 ili kupisha uchunguzi wa tuhuma zinazowakabili.
Bashungwa amechukua hatua hiyo wakati akikagua ujenzi wa hospitali ya wilaya Karagwe mkoani Kagera na kubaini ucheleweshwaji wa ujenzi wa majengo ya wodi ya wanaume, wodi ya wananamke, jengo la upausuaji na jengo la kuhifadhi maiti, chanzo chake kikiwa ni afisa manunuzi na mkaguzi wa ndani.
Bashungwa amesema Serikali ilitoa kiasi cha shilingi milioni 800 na zipo kwenye akaunti ya halmahauri kwa ajili ya ujenzi wa majengo manne lakini Afisa manunuzi amekuwa na michakato isiyokuwa rasmi na kuomba kupewa fedha ili atoe tenda kwa wazabuni na kuchelewa kufanya maamuzi ya ununuzi wa vifaa.
“Fedha zipo kwenye akaunti, sehemu ya tatizo ni Afisa manunuzi anapenda michakato na kuweka urasimu ili mzabuni ajiongeze ndio afanye maamuzi kwahiyo akae pembeni uchunguzi ufanyike kulingana na taratibu za kiutumishi,”amesema Bashungwa
Aidha, Bashungwa amesema Mkaguzi wa ndani ya halmashari amekuwa akishiriki kusambaza vifaa katika miradi ikiwa ni pamoja ujenzi wa majengo ya hospitali ya wilaya badala ya kusimamia thamani fedha zinazoletwa katika halmashauri hiyo.
Wakati huo huo, Bashungwa amewaagiza Wakurugenzi wa Halmashauri zote nchini kuhahikisha wanakamilisha miradi yote ya ujenzi wa miundombinu ya vituo vya afya, zahanati na hospitali za Wilaya ambayo mwisho wa utekelezaji (deadline) ni Juni 30 ilikuwa ikitekelezwa kabla ya fedha za Mapambano na Ustawi wa Taifa dhidi ya UVIKO- 19.
Nae, Mkuu wa Mkoa Kagera, Meja Jenerali Charles Mbuge amesemea katika eneo la mradi hakuna vifaa vya ujenzi kama matofari, mchanga na vifaa vingine ambayo vinachangia kuchelewa kwa ujenzi wa majengo hayo katika hospitali ya wilaya karagwe.