Breaking

Saturday, 25 June 2022

WATU WATANO WAFARIKI BAADA YA KUNYWA POMBE HARAMU INAYOSHUKIWA KUWA NA SUMU



Watu watano wamepoteza maisha yao baada ya kudaiwa kunywa pombe haramu katika kijiji cha Karuku, wadi ya Mwea Kitongoji cha Mbeere Kusini kaunti ya Embu Nchini Kenya.

Watano hao ni majirani, kati yao watatu walifariki dunia siku ya Jumatano Juni 22, 2022, na wengine wawili wakakata kamba Alhamisi 23, 2022.

Pia inaripotiwa kuwa wawili kati ya waliobugia pombe hiyo wamelazwa katika hospitali na inadaiwa wamepoteza uwezo wa kuona.

Kulingana na baadhi ya ripoti za polisi, mmoja wa marehemu alipokea KSh 35,000 (693460Tsh) za chama kutoka kwa marafiki zake na wakaingia kwenye ulevi.

Waliporejea nyumbani siku ya Jumatano wanaume wawili wanasemekana kuaga dunia, mmoja akifariki na wengine wakapoteza maisha yao Alhamisi, Juni 23.

Kamanda wa polisi wa Kaunti Ndogo ya Mbeere Kusini Gregory Mutiso alisema anafahamu watu watatu pekee ambao wameaga dunia akibaini kwamba walikuwa wamesafiri hadi Masinga huko Machakos kwa burudani.

Alisema baada ya kifo cha wawili hao, walianzisha uchunguzi na kuchukua sampuli za pombe walizokuwa wamekunywa kwa ajili ya kuzifanyia uchunguzi.

"Ninajua watu watatu pekee ambao wamefariki dunia tumechukua sampuli za pombe walizoripotiwa kunywa kwa uchunguzi zaidi," Mutiso alibainisha.

Alibainisha kuwa wanachunguza iwapo pombe hiyo haramu ilikuwa na sumu na kuongeza kuwa huenda marehemu walikula nyama ya mamba ambayo iliwaharibikia.

"Kuna ripoti ambazo tumepokea walikula nyama ya mamba wakirudi nyumbani na ni suala ambalo tunalichunguza pia," Mutiso aliongeza.

Inasemekana kuwa kabla ya kifo chao kutokea walikuwa wakilalamika kuhusu maumivu makali ya tumbo, kila mmoja akipoteza uwezo wa kuona na mwili kudhoofika.
Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia langolahabari@gmail.com au WhatsaApp: +255 621 896 990

Pages