Jeshi la Polisi mkoani Geita linawashikilia watu watatu kwa tuhuma za kujifanya maofisa wa Serikali na kutapeli viongozi wa Serikali wakiwamo wakuu wa wilaya na wakurugenzi.
Kamanda wa polisi mkoani Geita, Henry Mwaibambe amesema mfanyabiashara wa Dar es Salaam, Emanuel John (38) anashikiliwa kwa madai ya kujitambulisha kuwa ni Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Rais na kutapeli wakuu wa wilaya na wakurugenzi.
Amewataja watuhumiwa wengine kuwa Stanley George (34) mbeba mizigo mkazi wa Temeke na Musa Nasoro (35) dereva mkazi wa Mbagala, jijini Dar es Salaam.
Wawili hao pia wanakabiliwa na tuhuma za kujifanya maofisa wa Serikali na kutapeli viongozi.
Amewaambia waandishi wa habari kuwa Jeshi la Polisi mkoani humo lilianza kuwafuatilia baada ya kufanya mawasiliano na viongozi mbalimbali na kufuatilia mawasiliano ya watuhumiwa na kugundua kuwa wahusika walikuwa Dar es salaam.
Jeshi hilo lilifanikiwa kuwakamata kwa kushirikiana na polisi mkoani Dar es Salaam.
Amesema watuhumiwa wamekutwa na simu na laini nyingi zikiwa na majina ya viongozi waandamizi wa Serikali.
Mwaibambe amesema Emanuel amekua akipiga simu kwa viongozi akiwapa sifa kuonyesha Rais anaridhishwa na utendaji kazi wao, huku akiwataka waendelee kuwa karibu nae kwa kuwa yupo ofisi ya Rais.
Kamanda amesema watuhumiwa hao watafikishwa mahakamani wakati upelelezi utakapokamilika.
Source: Mwananchi