Na Lucas Raphael,Morogoro
TAASISI tatu za umma zinazojihusisha na uzalishaji wa mbegu nchini zimeazimia kuweka mkakati wa pamoja wa kuhakikisha wanamaliza tatizo la uingizaji wa ngano kutoka nje ya nchi .
Mkakati huo ambao uliokusudiwa utapelekea uzalishaji wa mbegu bora za zao hilo pamoja na usambazaji kwa wakulima nchini.
Akizungumza katika kikiao kazi cha siku moja kilichofanyika Mkoani Morogoro ambacho kimezikutanisha taasisi ambazo ni TARI, ASA na TOSCI Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania (TARI)Dkt Geofrey Mkamilo alisema kuwa katika mkakati huo wameangalia kila taasisi itafanya nini ndani ya miaka miwili ambayo ni maelekezo.
Dkt Mkamilo alisema kuwa ili kuhakikisha mkakati huo wa kuwa na mbegu bora za kilimo unafanikiwa wamekubaliana kuhakikisha wanakutana mara kwa mara ili kuangalia yutekalazaji wa waliyokubaliana na kuangalia changamoto zizo jitokeza na kuzitatua.
Hata hivyo alisema kuwa pamoja na makubaliano hayo ya kufanya kazi kwa kushirikiana kwa taasisi hizo tatu za umma lakini pia wameona ni vema kushirikiana na chuo kikuu cha kilimo cha Sokoine SUA ambapo alisema kuwa lengo ni kuhakikisha wanaboresha maswala mazima ya utafiti pamoja na upatikanaji wa mbegu bora.
Naye Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Mbegu za Kilimo ASA Dkt Sophia Kashenge alisema kuwa uzalishaji wa ndani ya nchi upo chini na kwamba ili kuweza kukidhi mahitaji ni lazima kuongeza uzalishaji wa mbegu.
Alisema kuwa uzalishaji wa ndani wa mbegu bado ni mdogo ambapo alisema kuwa kikao kazi hicho wameweka mkakati wa pamoja wa kuhakikisha wanafanya kazi kama timu ili kuongeza upatikanaji wa mbegu bora kwa wakulima.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Uthibiti Ubora wa mbegu Tanznia TOSCI ambaye pia ni mwenyekiti wa kikao kazi hicho Patrick Ngwediagi alisema kuwa taasisi hizo pia zimeingia mkataba wa hiari wa mashirikiano baina yao (MoU) ambao utaainisha majukumu ya kila taasisi kwa kuzingatia sheria zilizopo pamoja na matakwa ya kufanya kazi kwa pamoja.
“Makubaliano haya yanalenga kuhakikisha tunaongeza upatikanaji wa mbegu bora kwa watanzania”alisema
Hivyo alisema kuwa pamoja na mkataba huo wa hiari lakini pia wameingia makubaliano ya kuhakikisha wanakutana kila baada ya miezi sita ili kujadili mkakati waliouweka ikiwa ni pamoja na kujadili maswala yote yatakayojitokeza ambayo yanaboresha ushirikiano kwaajili ya kufanikisha upatikanaji wa mbegu bora nchini.
Alisema kuwa pamoja na kutoa majukumu kwa kila taasisi mkataba huo wa hiari utaweka taratibu za jinsi watakavyotekeleza mkakati ambapo alisema kuwa kila taasisi imepangiwa majukumu yake na kwamba isipofanya itawajibika,na kwamba wamekubaliana kuwa mkataba huo uandaliwe na uwe tayari ifikapo mwishoni mwa mwezi julai.
Mwisho