Breaking

Monday, 13 June 2022

WALIMU WAWILI WAFARIKI DUNIA AJALI YA PIKIPIKI NA GARI - KENYA


Walimu wawili wa shule ya Sekondari Kiini Girls wamefariki dunia katika ajali ya barabarani kwenye barabara ya Sagana-Karatina kaunti ya Kirinyaga Nchini Kenya.


 Akithibitisha ajali hiyo Mkuu wa polisi katika kaunti ndogo ya Kirinyaga Magharibi David Kabina, amewataja Walimu hao kuwa ni Muriuki Ndambiri (42) na Elasmus Maina Mwita (37) ambao walikuwa wakielekea nyumbani kutoka mji wa Sagana usiku wa kuamkia leo Jumatatu Juni 13, 2022 walipogonga gari lililokuwa likitoka upande tofauti.


Kabina amesema kuwa  pikipiki waliyokuwa wamepanda ilipogongana na gari katika kijiji cha Kiangwaci eneo bunge la Ndia ambapo mara tu baada ya ajali hiyo kutokea, dereva wa gari hilo alikimbia.


Amesema Jeshi la Polisi bado linamsaka dereva huyo na akikamatwa atafunguliwa mashtaka ya kusababisha kifo kwa kuendesha gari bila kufuata sheria.


Aidha, Kabina ametoa wito kwa wananchi kutoa ushirikiano kwa polisi na taarifa za kujitolea zitakazofanikisha kukamatwa kwa dereva huyo.

 "Hatutapumzika hadi dereva aliyesababisha vifo akamatwe na kufunguliwa mashtaka," amesema.


Ameongeza kuwa miili ya walimu ilipelekwa katika hifadhi ya maiti ya hospitali ya Murang’a huku pikipiki ikikokotwa hadi kituo cha polisi cha Sagana.


Mashuhuda wa tukio hilo walisema waliona gari lililokuwa katika mwendo kasi likiyumba kabla ya kugongana na pikipiki hiyo uso kwa uso na kusababisha kifo cha walimu hao.


 "Ilikuwa ajali mbaya ambayo iliua walimu hao vijana wawili kutoka eneo hilo," mmoja wa wakazi alisema.

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia langolahabari@gmail.com au WhatsaApp: +255 621 896 990

Pages