Breaking

Friday, 24 June 2022

WAHADHIRI CONAS WATAKIWA KUFANYA TAFITI



Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam 


WAHADHIRI na wanafunzi wa Ndaki ya ya Sayansi Asili na Sayansi Tumizi (CoNAS), ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), wameshauriwa kufanya tafiti ambazo zitaweza kuchochea ukuaji wa uchumi na maendeleo kwa jamii.

Ushauri huo umetolewa na Mkurugenzi wa Shahada za Awali UDSM Profesa Nelson Boniface wakati akizungumza na vyombo vya habari katika mwendelezo wa sherehe za miaka 60 tangu kuanzishwa chuo hicho, zinazotarajiwa kufikia kilele Oktoba mwaka huu.

Prof. Boniface ambaye alimwakilisha Makamu Mkuu wa Chuo UDSM, Profesa Willium Anangisye, alisema ili nchi na jamii iendelea nyenzo muhimu inayotumika ni kufanya tafiti ambazo zinatatua changamoto zilizopo.

Alisema historia inaonesha kuwa wahadhiri na wanafunzi wa ndaki hiyo wamekuwa wakifanya tafiti ambazo zinachangia maendeleo ya jamii, ila bado wanatakiwa kuongeza juhudi katika eneo hilo muhimu.

“Nchi yoyote ambayo imeendelea duniani msingi mkubwa ni utafiti, hivyo mnapofanya utafiti, hakikisheni unaleta manufaa katika uchumi, maendeleo na jamii katika nchi yetu. Kama utafiti mnaofanya hauegemei katika mambo hayo mawili, basi utakuwa hauna maana,” alisema.

Mkurugenzi huyo alisema pamoja na hayo ni vema wahadhiri hao kuhakikisha tafiti wanazofanya hazifungiwi kabatini pindi zinavyokamilika na kwamba hazitakuwa na maana.

Prof, Boniface alisema CoNAS ilianzishwa mwaka 1965, miaka minne baada ya kuanzishwa kwa UDSM, hivyo ni vema umri wa uwepo wake uweze kutoa matokeo chanya kwa jamii ya Kitanzania.

“Ndaki hii imekuwa ikifanya tafiti nyingi ikiwemo utafiti wa mafuta katika mimea, uyoga na nyingine ambazo kwa pamoja zinaenda kumkomboa Mtanzania. Ila kwa sasa anzeni kujikita kwenye utafiti wa ubunifu na sayansi za maendeleo,” alisema.

Kwa upande wake Mkuu wa Ndaki ya CoNAS, Prof. Flora  Magige, alisema kwa miaka zaidi ya 56 ya uwepo wa ndani hiyo wamekuwa wakifanya tafiti mbalimbali ambazo zimechangia mapinduzi ya kiafya, kiuchumi na maendeleo.

“Tumefanya tafiti nyingi hapa CoNAS, ila tafiti ambayo tunaendelea kujivunia hadi sasa ni hii ya kugundua dawa ya kutibu Uviko-19 iitwayo Yudano ambayo imewatibu wagonjwa wengi wakati wa mlipuko wa ugonjwa huo,” alisema.

Alisema dawa ya Yudano imeweza kusaidia watu wengi kupona, na mpaka sasa bado inaendelea kuuzwa katika maeneo mbalimbali nchini.

Mkuu huyo wa ndaki alisema wanaendelea na tafiti mbalimbali ambazo zitaweza kutatua changamoto zinazowakabili wananchi hasa wa kipato cha chini.

“Tutarajie kuona mambo makubwa kutoka kwenye ndaki hii, kwa kuwa ubunifu unaendelea na maandiko yanaendelea ambayo yataleta uvumbuzi wa mambo mbalimbali,” alisema.

Ndaki ya Sayansi Asili na Sayansi Tumizi kwa siku za karibuni imekuwa ikibua wanafunzi wabunifu ambao wamekuwa wakishinda katika mashindano mbalimbali ya bunifu za kisayansi ikiwemo za njia ya bioteknolojia.
 

Mwisho
Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia langolahabari@gmail.com au WhatsaApp: +255 621 896 990

Pages